Breaking News

TANROADS YATANGAZA MAFANIKIO YA SERIKALI MIAKA MINNE YA SAMIA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma - Mkurugenzi wa Wakala ya Mipango ya Miundombinu (TANROADS) Ephatar Mlavi amesema Serikali imefanikisha kujenga mtandao wa barabara za lami, madaraja na viwanja vya ndege kwa kipindi cha miaka minne ya Awamu ya Sita.

Mlavi amesema hayo leo Februari 17, 2025 alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo ya wakala huo kwa kipindi cha miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema kwa kipindi hicho barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 15,625.55 zimekuwa katika hatua mabalimbali za utekelezaji ambapo barabara zenye urefu wa kilometa 1,365.87 zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami.

Pia barabara zenye urefu wa kilometa 2,031.11 zimeendelea kujengwa kwa kiwango cha lami.

 "Aidha, barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 2,052.94 na madaraja mawili zimefanyiwa Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina na Serikali inatafuta fedha za kuzijenga kwa kiwango cha lami. 

"Vilevile, Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina wa barabara zenye jumla ya kilometa 4,734.43 na madaraja 10 unaendelea.

Amesema miradi ya barabara yenye urefu wa takriban kilometa 5,326.90 na miradi saba ya madaraja ipo katika hatua ya manunuzi kwa ajili ya kufanyiwa Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina ikiwa ni maandalizi kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara hizo kwa kiwango cha lami. 

"Katika kipindi tajwa madaraja makubwa tisa yamekamilika kujengwa kwa gharama ya Sh. Bilioni 381.301," amesema.

Ameyataja madaraja hayo kuwa ni Gerezani (Dsm), Daraja jipya la Tanzanite (Dsm), Wami (Pwani), Kitengule (Kagera), Kiyegeya (Morogoro), Ruaha (Morogoro), Ruhuhu (Ruvuma), Mpwapwa (Dodoma) na daraja la Msingi (Singida). 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji mkuu wa Serikari Greyson Msigwa,amewataka wakuu wote wa Taasisi za Serikali kuhakikisha wanatoa taarifa zao za utekelezaji wa shughuli za maaendeleo.

No comments