Breaking News

IRENE ISHENGOMA AIMWAGIA SIFA MTANDAO WA WANAWAKE LAKI MOJA KWA KUIBUA VIPAJI SOKA LA WANAWAKE TEMEKE

Na. Andrew Chale, Temeke. - Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Chama Cha Mpira wa miguu kwa Wanawake Tanzania (TWFA) ambaye pia ni mdau wa michezo nchini, Bi. Irene Ishengoma ameipongeza Mtandao wa Wanawake Laki Moja kwa kuwezesha kufanyika ligi ya soka kwa Wanawake ndani ya Temeke iliyopewa jina la Wanawake Laki Moja Cup 2025.

Irene Ishengoma pia ni Kocha ngazi ya CAF, Mratibu Mkuu Wa Utekelezaji wa Mradi wa “Ukatili michezoni haukubariki” wenye lengo la kupinga ukatili kwa Wanawake Michezoni na Afisa tathmini na Ufatiliaji GPF (Global Peace Foundation Tanzania), ambaye alikuwa mgeni rasmi katika fainali za ligi hiyo ya Wanawake Laki Moja Cup mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Buliyaga Temeke, amesema kuwa kitendo cha taasisi hiyo kupitia kwa mlezi wake Mhe DC Mstaafu Tano Mwera kudhamini michezo ya soka la Wanawake ni cha kuungwa mkono kwani kinaleta faraja kwa Wanawake na kutambua michezo kama njia ya ajira.

"Najivunia sana kiongozi mlezi wa Wanawake Laki Moja, Mama Tano Mwera, Dada Mwanaharusi Kingwendu Mratibu wa mashindano haya, Viongozi wa mpira wa miguu kwa Wanawake Temeke (TEWFA)Bw. Yasin Nonji na wengine wote hakika wamefanya jambo kubwa na la kihistoria kwa mabinti hawa.
Lakini pia kipekee nipongeze TFF, TWFA, kwa kuendelea kusongesha mbele gurudumu la maendeleo ya soka la Wanawake Tanzania ndio maana wadau wanazidi kujitokeza na kufanya mambo makubwa ikiwemo kudhamini mashindano kama walivyofanya Wanawake Laki Moja." Amesema Irene Ishengoma.

Aidha, Irene Ishengoma amewataka Wadau wa soka la Wanawake kuendelea kuunga mkono michezo hiyo ikiwemo kuwashika mkono ilikuendelea kuibuka vipaji vingi kwani soka ni ajira kwa sasa na Tanzania imekua Moja ya Nchi zinazoendelea kufanya vyema katika soka hilo kwa Wanawake.

Kwa upande wake, Mhe. DC Mstaafu Tano Mwera Mlezi wa Mtandao huo wa Wanawake Laki Moja na mdhamini wa Ligi hiyo ya Wanawake Laki Moja Cup 2025, amewapongeza Waratibu wa mashindano hayo na kuwaahidi kuendelea kuwashika mkono katika jambo la michezo kwani Soka ni ajira.
Tunashukuru kwa kumaliza salama jambo letu tumehitimisha leo. Hongera wote walioshiriki na Walioshinda, niwapongeze Temeke Sisters kwa ushindi wenu,
Lakini pia Asanteni kwa timu zote shiriki na Na wadau wote mlioshiriki kwa njia moja au nyingine Nawapenda sana. “Cheza Soka Kama Mwanamke Soka ni Ajira”. 

Mtandao wa Wanawake Laki Moja milango ipo wazi kwa wadau na Waratibu wa Soka la Wanawake karibuni tupo tayari kushirikiana". Amesema Mhe DC Mstaafu Tano Mwera. 

Aidha, katika fainali hiyo, Timu ya Temeke Sisters iliweza kuibuka mabingwa kwa ushindi wa bao tatu kwa mbili dhidi ya Sayari Women.

Ambapo mshindi wa kwanza aliweza kukabidhiwa Tsh 500,000 taslimu, huku wa pili akipata Tsh 300,000 na kwa mshindi wa tatu amepata Tsh 200,000 na Nne alipata Tsh 150,000.



No comments