Breaking News

RC CHALAMILA AFANYA ZIARA KIWANDA CHA SARUJI WAZO HILL

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila amefanya ziara katika kiwanda cha Saruji cha Wazo Hill Wilaya ya Kinondoni kufatia malalamiko ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakitolewa na uongozi wa kiwanda hicho.

Akizungumza mara baada ya kuwasili kiwandani hapo RC Chalamila amesema kumekuwepo na malalamiko juu ya uvamizi wa eneo la kiwanda jambo ambalo limepelekea kiwanda kuwa na eneo dogo licha ya kuwa na eneo kubwa hapo awali hivyo kusababisha kuwepo kwa changamoto ya mifumo ya upatikanaji wa maji toshelevu kwa matumizi ya kiwanda.

Aidha katika kufikia suluhu ya malalamiko hayo RC Chalamila amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kuitisha mkutano wiki ijayo ambao utajumuisha wananchi wa eneo hilo, uongozi wa Mkoa na Wilaya pamoja na uongozi wa kiwanda ili kuanza upya mazungumzo, pia amemtaka Mtendaji mkuu DAWASA kufika mara moja katika kiwanda hicho kuketi na menejimenti ya kiwanda hicho ili kuona namna bora ya kumaliza changamoto hiyo.
"Namwagiza Mtendaji mkuu DAWASA na timu yake kufika mara moja katika kiwanda hapa kuketi na menejimenti ya kiwanda ili kuona namna bora ya kumaliza changamoto hiyo". Alisema RC Chalamila.

Katika hatua nyingine RC Chalamila amemuagiza Naibu kamisha wa Ardhi Mkoa kwa kushirikiana na wanasheria chini ya usimamizi wa Katibu Tawala wa Mkoa kuunda kamati ndogo ambayo itapitia malalamiko na hukumu zilizotolewa na mahakama katika eneo hilo ili kuweza kumshauri Mkuu wa Mkoa njia sahihi za kupita kwa lengo la kupunguza malalamiko kwa mwekezaji.

Sanjari na hilo RC Chalamila amesema Kiwanda hicho ni muhimu sana kwa masilahi mapana ya umma kwa kuwa kinatoa fursa kubwa ya ajira lakini pia huchangia katika pato la Taifa.



No comments