2025 NI MWAKA WA UAMUZI NA MAGEUZI YA KWELI - MCHINJITA
Dar es salaam - Waziri Mkuu Kivuli wa ACT Wazalendo, Ndugu Isihaki Rashidi Mchinjita, ameeleza kuwa baraza kivuli litatumia mwaka 2025 kusimamia haki za wananchi, uwajibikaji wa Serikali na kupigania mageuzi ya kweli ya kidemokrasia.
Mchinjita amesema mwaka 2024 ulikuwa wa mateso makubwa hasa kutokana na migogoro ya ardhi, kasi ya kukua kwa deni la serikali, hali mbaya ya kiuchumi, kuongezeka kwa matukio ya utekaji na mauaji, maafa ya mvua za Elnino na kushindwa kwa serikali kutoa huduma bora kwa wananchi. Ameeleza kuwa mwaka 2025 haupaswi kuendelea kutoa mateso tena.
Katika kusisitiza msimamo huo, amesema kuwa Watanzania wanapaswa kushirikiana na ACT Wazalendo kufanya maamuzi yatakayoleta mabadiliko katika kuimarisha maisha yao na kujenga taifa la wote.
Kauli hiyo ameitoa leo Jumatano Januari 8, 2025 akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama, Magomeni, Dar es Salaam wakati akitoa tathmini ya mwaka 2024 na kuelezea mwelekeo wa Baraza hilo kwa mwaka 2025.
"Mwaka 2025 ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu ni mwaka wa uamuzi. ACT Wazalendo tumejizatiti kuimarisha haki za kijamii, kupigania mageuzi ya demokrasia na maendeleo ya kiuchumi kwa maslahi ya wote."
Aidha, Waziri Mkuu Kivuli amesema mwaka 2024 ulikuwa na changamoto ya hali mbaya ya kiuchumi, ambapo deni la serikali lilishuhudia kupaa na kufikia shilingi trilioni 93.7. Hali ambayo imeathiri uwezo wa serikali kutoa huduma bora na kuajiri watumishi wa kutosha katika sekta muhimu kama afya na elimu. Pia, tatizo la vijana kukosa ajira limechangia ugumu wa maisha.
Kwa upande mwingine, amesema kuwa moja ya changamoto kubwa zilizoathiri Watanzania mwaka 2024 ni migogoro ya ardhi, ambayo imesababisha maumivu makubwa kwa wananchi wanyonge.
“Tangu kuingia madarakani Rais Samia Suluhu Hassan kumeibuka kwa kasi ya ajabu ya wimbi la uporaji wa ardhi katika maeneo mbalimbali nchini. Wimbi hili limeenda sambamba na ukatili uliopindukia wa kupora mali, mauaji ya raia, matumizi ya nguvu kuhamisha wananchi katika maeneo yao na kusogeza mipaka ya hifadhi kwenye mipaka ya vijiji.” alisema Mchinjita.
Kuhusu hali ya huduma za kijamii, Waziri Mkuu Kivuli ameonesha kusikitishwa na gharama kubwa za matibabu na mfumo wa bima ya afya usio na usawa. Alisisitiza umuhimu wa kuwaunganisha wananchi katika mfumo wa hifadhi ya jamii kutoa uhakika na kuzingatia mahitaji ya wananchi wote bila kujali uwezo wao wa kifedha.
“Ni jambo la aibu kuona wananchi wa kipato cha chini wakinyimwa huduma za afya kwa sababu hawawezi kumudu gharama. Afya ni haki, si bidhaa,” aliongeza.
Katika hotuba yake, Waziri Mkuu Kivuli alilaani ongezeko la matukio ya utekaji, kupotea, na mauaji ya raia wasio na hatia nchini huku Jeshi la Polisi likiwa kimya bila kuchukua hatua madhubuti. Ameongeza kuwa watuhumiwa wakubwa wa vitendo hivyo ni vyombo vya ulinzi na usalama hasa Idara ya usalama wa taifa na Jeshi la Polisi.
Akizungumzia demokrasia, Waziri Mkuu Kivuli alisisitiza hitaji la kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi, akibainisha kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 umeonesha sura halisi ya Rais Samia kuwa hataki mageuzi, kauli za R4 ni hadaa.
“Ili tuwe na uchaguzi wa haki na uwazi mwaka 2025, ni lazima tuwe na Tume Huru ya Uchaguzi itakayohakikisha kila kura ya Mtanzania inaheshimiwa,” aliongeza.
Amehitimisha kwa kuahidi kuwa Baraza Kivuli litaendelea kuwa sauti ya wananchi, huku ikisisitiza mshikamano wa kitaifa kupambana na changamoto zilizopo. Huu ni mwaka wa kuchukua hatua thabiti. Tanzania inastahili zaidi ya haya tunayoshuhudia sasa. Ni wakati wa kuleta mageuzi ya kweli.
No comments