Breaking News

UFUGAJI KUKU AINA YA 'BROILA' NI SULUHISHO LA UHABA WA PROTINI

 

Dar es Salaam, Mtafiti na mtaalam wa ufugaji Kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe Proscovia Kamugisha amesisitiza umuhimu wa kuongeza ufugaji wa kuku aina ya 'Broila' ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa chakula chenye protini nchini. 

Akizungumza katika Kongamano la Tisa la Wanasayansi, Watafiti, na Wabunifu, Bi. Kamugisha ameeleza kuwa ufugaji wa kuku wa aina hii ni suluhisho rahisi na lenye tija.

"Ufugaji wa kuku aina ya 'Broila' huchukua muda mfupi, hii husaidia kuwa na uhakika wa upatikanaji wa chakula chenye chanzo cha protini katika nchi yetu," amesema. Kuku wa 'Broila' wanakua haraka, huchukua wastani wa wiki tano kufikia hatua ya kuchinjwa, na hivyo kutoa suluhisho la haraka kwa mahitaji ya chakula.

Kamugisha ameongeza kuwa kuimarisha uzalishaji wa 'Broila' kutasaidia kuongeza upatikanaji wa nyama ya kuku kwa wingi na kwa gharama nafuu, hali itakayosaidia familia nyingi kuwa na uwezo wa kumudu lishe bora. "Ni muhimu sana kuongeza kiwango cha ufugaji wa aina hii ya kuku kwani itasaidia upatikanaji wake kwa wingi na kwa gharama nafuu," alisisitiza.

Kwa mujibu wa Bi. Kamugisha, jitihada za kuendeleza ufugaji wa 'Broila' zinapaswa kuungwa mkono kwa kuwezesha wakulima wadogo kwa mafunzo, mtaji, na upatikanaji wa mbegu bora za kuku. Pia, ameiomba serikali kushirikiana na sekta binafsi katika kuboresha miundombinu kama maghala ya kuhifadhia chakula na masoko ya uhakika.

Kauli ya Bi. Kamugisha inaendana na maudhui ya kongamano hili, "Matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa Ustahimilivu wa Tabianchi na Uchumi Shindani." ikilenga kutumia ubunifu wa kisayansi katika kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.

No comments