SEKTA YA HABARI NI NGUZO MUHIMU KATIKA KUIMARISHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO, INAPASWA KUHESHIMIWA - PROF. KABUDI.
Dar es salaam - Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema kuwa vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kujenga taswira ya taifa, demokrasia, uwazi, uwajibikaji, na maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Ametoa wito kwa vyombo vya habari kupewa nafasi maalum, huku akisisitiza kuwa serikali inatekeleza wajibu wake wa kuhakikisha sekta ya habari inaimarika.
Prof. Kabudi ameweka bayana mafanikio ya serikali ya awamu ya sita kupitia dhana ya 4R (Reconciliation (Maridhiano), Resiliency (Ustahimilivu), Reforms (Maboresho), Rebuilding (Ujenzi wa Upya) ambayo imeongeza mashirikiano kati ya serikali na sekta mbalimbali ikiwemo ya habari.
Prof. Kabudi ameyasema hayo Disemba 18,2024 katika mkutano wake na wadau wa Sekta ya Habari na Utangazaji na kuzungumza mambo mbalimbali yanayohusu sekta ikiwemo changamoto zinazoikabili na mafanikio yake.
Amesema kuwa kutokana na jitihada mbalimbali za serikal kuhakikisha inadumisha uhuru wa habari Tanzania imepanda katika viwango vya kimataifa vya uhuru wa vyombo vya habari, kutoka nafasi ya 143 mwaka 2023 hadi nafasi ya 97 mwaka 2024.
Ameongeza kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha sera ya habari ya mwaka 2003 inafanyiwa maboresho ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya sasa. Waziri Kabudi amewahimiza waandishi wa habari kuwa wabunifu, kuandika kwa weledi, na kuzingatia uhalisia wa taarifa wanazochapisha, ili kuepuka kuandika habari zisizo za uhakika au zenye upendeleo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa, amesema kuwa serikali imefanya juhudi mbalimbali kuboresha sekta hiyo, ikiwemo maboresho ya sheria za habari, mifumo ya kielektroniki na huduma za posta, pamoja na kuunda kamati ya uchumi wa vyombo vya habari na wanahabari ambayo tayari imeshawasilisha ripoti yake inayongoja kupitiwa na kufanyiwa kazi.
Bw. Msigwa amesisitiza umuhimu wa kushirikiana na wadau katika mijadala inayolenga kuboresha sekta hiyo ili iweze kuchangia maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt.Jabiri Bakari amesema mamlaka hiyo imetoa leseni 250 za redio, 40 za televisheni za bure, 29 za televisheni za kulipia na 206 za redio na televisheni za mtandaoni. Huku leseni 4 walitoa kwa watoa Huduma ya miundombinu kidigital, na Leseni Mbili za watoa huduma kupitia Satellite.
Hatua hizo zimeimarisha upatikanaji wa habari na kuongeza jukwaa la utoaji wa taarifa kwa wananchi.
Nae Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kamati ya Maudhui kutoka Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari amesema bodi hiyo inalenga kuimarisha weledi wa waandishi wa habari ili kuboresha ubora wa taarifa.
Baraza la Habari Tanzania, kupitia Katibu Mtendaji wake Bw. Ernest Sungura, limepongeza juhudi za serikali, huku likitangaza kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa mabaraza ya habari duniani, utakaolenga kudumisha uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kupata taarifa.
Katibu Mkuu wa Jumuia ya Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), Bw. Suleiman Msuya, ameainisha changamoto zinazowakabili waandishi wa habari, ikiwa ni pamoja na mishahara midogo, kutokuwa na mikataba ya kazi, na ukosefu wa bima za afya.
Nae, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Bw. Deodatus Balile, amesisitiza umuhimu wa mazungumzo ya mara kwa mara kati ya serikali na wadau wa habari ili kuhakikisha sekta hiyo inaimarika na kuepusha mivutano kati ya Serikal na vyombo vya habari na Waandishi wa habari.
Aidha Waziri Kabudi ameagiza Bodi ya Ithibati kuhakikisha changamoto za waandishi zinashughulikiwa, huku akihimiza waandishi kupata mafunzo ya mara kwa mara ili kuboresha taaluma yao. Serikali imeahidi kuendelea kushirikiana na wadau wa habari katika kujenga sekta thabiti, yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa
No comments