“HATUTAKI TUWE WENYEJI WA CHAN NA AFCON HALAFU TUTELEWE MAPEMA
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na michezo, Mhe Hamis Mwinjuma amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau imedhamiria kuiandaa timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu (Taifa Stars) ili kuvunja rekodi ya kutokuvuka hatua ya awali kwenye mashindano ambayo Tanzania ni mwenyeji ikishirikiana na Kenya na Uganda.
Mhe. Mwinjuma ameyasema hayo leo 21 Desemba 2024 Mjini Moshi alipokuwa akifungua Mkutano wa 19 wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambapo amewataka wadau kuungana pamoja kwenye maandalizi ya timu ya Taifa ya miguu hasa inapokwenda kushiriki mashindano ya Afrika kama wenyeji ili kipindi hiki kiwe ni cha kuweka historia kwani itakuwa ajabu mwenyeji kutolewa hatua za awali.
“Tunapokwenda kuandaa CHAN na AFCON kuna ushiriki wetu wa aina mbili, wa kwanza ushiriki kama waandaaji ambapo kwa sehemu kubwa Serikali inafanya jukumu lake la kujenga miundombinu na kuhakikisha kila kinachohitajika kinafikiwa na hakuna mahali tunakwama, la pili ushiriki wetu kama washiriki tunaokwenda kucheza, litakuwa jambo la ajabu tunaandaa AFCON halafu tukawa watu wa kwanza kutolewa”-Amesema Mhe Mwinjuma
“Tunashiriki AFCON lakini hatujawahi kuvuka raundi ya awali, mimi kwa nafasi niliyonayo kwa kushirikiana na ninyi TFF na wajumbe wa mkutano huu ambao mnaoendesha mpira wa miguu kote nchini moja ya malengo yangu makubwa ni kuhakikisha tunavunja rekodi hii hatuishii tena raundi ya kwanza”. Amesema mhe Mwinjuma
Aidha Mhe. Mwinjuma amewapongeza Wajumbe wa Mkutano Mkuu chini ya Rais Karia kwa mafanikio makubwa ambayo yamepatikana mwaka huu kwa timu za Taifa (Taifa Stars) kufuzu AFCON 2025, Twiga Stars kwa kufuzu WAFCON 2025, timu ya U20 (Ngorongoro Heroes) kwa kufuzu AFCON ya U20, na timu ya wavulana ya U15 kuibuka mabingwa wa michuano ya shule ya Afrika chini ya CAF ambayo fainali zake zilifanyika Mei 2024 kisiwani Zanzibar.
Mhe Mwinjuma ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kushirikiana na TFF kuhakikisha timu za Taifa pamoja na klabu zinafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
Mkutano huo wa kila mwaka umewakutanisha wajumbe kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara, vyama shirikishi, na klabu za Ligi Kuu ya NBC. Katika mkusanyiko huo ndipo mipango ya maendeleo inawasilishwa, kujadiliwa na baadaye kupitishwa kwa ajili ya utekelezaji.
No comments