Breaking News

KAMATI YA BUNGE, PIC YARIDHISHWA NA UWEKEZAJI WA SERIKALI VIWANJA VYA NDEGE NCHINI

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imesema imeridhishwa na uwekezaji unaofanywa na Serikali kwenye Ujenzi wa Viwanja vya Ndege nchini.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam 15 Novemba 2024 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe Augustine Vuma mara baada ya Kamati hiyo kupewa semina ya shughuli za Ujenzi,Uendeshaji na Utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).

Mhe. Vuma amesema kupitia Uwekezaji uliofanywa na Serikali ni wakati muafaka wa Bodi na Menejimenti ya TAA kufikiria namna itakavyopata vibali vya kutumia mapato ya ndani kuendelea Miradi ya Ujenzi na kujilipa mishahara.

“Uwekezaji uliowekwa na Serikali kwa TAA umeonyesha matokeo sababu mmesikia hapa taarifa inaonyesha kwenye mapato yanayokusanywa kuna fedha zinabaki kama bakaa ambalo inawezekana kuiomba Serikali fedha hizo zitumike kwenye Miradi ya maendeleo” amesema Mhe. Vuma.
Mhe. Vuma amesema Mamlaka za Serikali zinakuwa na Nguvu zaidi pale zinapokusanya mapato na kujilipa mishahara kupitia mapato yanayokusanywa ndani ya Taasisi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi Mhe. David Kihenzile amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuboresha Viwanja vya Ndege Nchini ambapo matokeo ya Uwekezaji ni kuchagiza Uchukuzi kwa njia ya Anga.

Naibu Waziri Kihenzile ameongeza kuwa matokeo ya maboresho hayo ni pamoja na ongezeko la safari za ndege, idadi ya Masharika yanayofanya safari zake kupitia Viwanja vya Ndege vya Nchini, mizigo pamoja na Abiria.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA Hamisi Amiri ameishukuru Serikali kwa kubadilisha Sheria ya TAA ambapo mabadiliko hayo yataboresha utendaji wa Mamlaka.

No comments