Breaking News

DKT BITEKO AWATAKA WAHITIMU WASIOGOPE CHANGAMOTO ZA MAISHA BAADA YA CHUO

📌 Awahimiza kufanya uamuzi sahihi, kujibu maswali na dukuduku walizonazo

📌 Apongeza ushirikiano wa Serikali na Sekta Binafsi katika maendeleo nchini*

📌 SAUT yamshukuru Rais Dkt. Samia kwa miongozo katika sekta ya elimu
 
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewahimiza wahitimu katika ngazi mbalimbali kutumia taaluma yao kufanya maamuzi sahihi yatakayowawezesha kupata majibu ya maswali na dukuduku walizonazo kuelekea maisha mapya.

Dkt. Biteko ametoa rai hiyo Novemba 16, 2024 katika Mahafali ya 13 ya Chuo Kikuu Kishiriki, Stella Maris cha Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino, Mtwara. 

Pamoja na kuwapongeza wahitimu kwa kuhitimu amewataka kutumia taaluma waliyoipata kuwa nyenzo katika utatuzi wa changamoto watakazokabiliana nazo maishani baada ya kuondokana na maisha ya chuo. 

“Wengine wanaendelea kujiuliza, nini kitafuata baada ya kuhitimu? Uelekeo utakuwa ni upi? na wengine wanasema hali sio nzuri huko tuendako. Kila wakati endelea kuwa tofauti, kila mtu ana njia yake ya kuishi, tumia taaluma mliyoipata kwa maamuzi sahihi. Amini vyeti pekee havitoi maarifa bali endeleeni kujifunza kwa waliowatangulia”, amesema Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko amewapa shime wahitimu na kuwataka wasisikilize sauti za baadhi ya watu wenye nia ya kuwavunja moyo kwa vitisho na kauli za kukatisha tamaa kuhusu maisha baada ya kuhitimu elimu ya Chuo. 

“Acheni kusikiliza kauli za wavunja moyo bali fuata sheria, tenda haki na kumjenga mwenzako kimaisha na kisaikolojia’’amesema Dkt. Biteko.

Katika hatua nyingine, amewataka wahitimu kujipanga na kukabiliana na matokeo ya ushindani pamoja na matishio mbalimbali ya kidunia ikiwemo mabadiliko ya teknolojia na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi kama vile ongezeko la joto duniani, ongezeko la idadi ya vimbunga, ukame, njaa na matetemeko ya ardhi.

Awali, mgeni rasmi amesema serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inathamini mchango wa sekta binafsi katika kuchochea maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwamo sekta ya elimu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho, Mhashamu Askofu Titus Mdoe ameishukuru Serikali kwa kutoa kibali, miongozo na ushauri katika uendelezaji wa shughuli za elimu jambo linalowezesha utekelezaji wa malengo waliojiwekea.

“Tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suhuhu Hassan pamoja na viongozi wengine kwa ushirikiano tunaoupata kutoka ngazi ya wilaya hadi Taifa.” Amesema Askofu Mdoe.

Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Chuo ambaye alimwakilisha Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mt. Agustine, Mhashamu Askofu Wolfgang Pisa ameiomba Serikali kuwashika mkono wanafunzi wa Chuko Kikuu Kishiriki cha Stella Maris ili waweze kutatua changamoto za maisha wanapokuwa chuoni.

Naye Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Stella Maris Mtwara, Padri, Profesa Thadeus Mkamwa amesema elimu inayotolewa katika chuo hicho kuwajengea wanafunzi uwezo na umahiri katika utatuzi wa changamoto wanazokabiliana nazo.
Pia amesema wanachuo wanafundishwa misingi ya upendo, uvumilivu pamoja na kuwajengea vijana mifumo ya ubunifu kwa ajili ya kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Jumla ya wanachuo 581 wamehitimu wakiwemo wa ngazi ya astashahada, stashahada pamoja na shahada ikiwa ni sawa na asilimia 83 ya waliostahili kuhitimu huku wanafunzi 117 wakishindwa kuhitimu kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ada.





 

No comments