ACT INAPIGANIA HAKI ZA WATU WOTE
Mheshimiwa Othman, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo leo Novemba 03, 2024 wakati akizungumza na Wananchi katika Viwanja vya Jaribu Mpakani, Jimbo la Kibiti Mkoa wa Pwani,
"Kibiti imekuwa maarufu leo, si kwa sababu ya korosho au mananasi yao, bali ni kutokana na madhila waliyoyapata Wananchi yakiwemo mauaji na ukandamizaji dhidi ya haki zao." Alisema Mheshimiwa Othman.
Mheshimiwa Othman pia amefahamisha kwamba iwapo kuna Malalamiko ya Wananchi kufuatia Kutoweka kwa Ndugu na Jamaa zao, Mamlaka husika zinapaswa kutafuta ufumbuzi, na wala siyo kukaa kimya, kuleta visingizio na au ubabaishaji.
Hata hivyo, Mheshimiwa Othman ameahidi kwamba, yeye na Safu ya Viongozi wenzake wa ACT-Wazalendo, kama ilivyo Itikadi yao ya Tanzania ya Wote kwa Maslahi ya Wote, watahakikisha wanasimama na Wananchi wote, katika kupigania na kutetea haki zao.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho upande wa Tanzania Bara, Ndugu Isihaka Mchinjita, amesema licha ya kuwa Mkoa wa Pwani kujaaliwa rasilimali nyingi, zikiwemo za mazingira bora ya uzalishaji wa Mazao ya Biashara, lakini wakaazi wake wote, wamekuwa kielelezo cha Jamii ya Watu Maskini, hapa Nchini.
Awali kabla ya Mkutano huo Mheshimiwa Othman alipata fursa ya kuzungumza na Viongozi pamoja na Wagombea wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kutoka ACT- Wazalendo katika Ukumbi wa Jaribu Mpakani, Jimbo la Kibiti.
Mheshimiwa Othman, anaendelea na Ziara yake katika Mkoa wa Mwambao na Pwani iliyojumuisha Shughuli mbali mbali za Serikali, Siasa na Jamii.
No comments