Breaking News

WAANDISHI WA UHIFADHI WASEMA VYOMBO VYA HABARI VINA WAJIBU WA KUILINDA HIFADHI YA NGORONGORO

Na Mwandishi wetu.
Baadhi ya waandishi wa habari wa masuala ya uhifadhi wamesema kuwa vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kuhakikisha hifadhi ya Ngorongoro inalindwa kikamilifu ili iendelee kuwa kivutio cha watalii kutoka nchi mbalimbali duniani.

Wakizungumza mara baada ya kutembelea hifadhi hiyo ili kujionea hali halisi ya uhifadhi waandishi wa habari hao wamesema serikali isipochukua hatua madhubuti kulilinda eneo hilo litapotea kutokana na kuwa na idadi kubwa ya watu na mifugo.

Bwana Manyerere Jackton kutoka gazeti la Jamhuri amesema watanzania ni lazima waungane na wawe na utashi wa pamoja katika kuhakikisha kuwa Ngorongoro inalindwa hasa kutokana na idadi ya watu kuongezeka kutoka watu elfu nane mwaka 1959 hadi kufikia zaidi ya watu laki moja kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022.
Kwa upande wake Mwandishi wa habari Mkongwe wa kujitegemea bwana Salim Said Salim amesema kuwa amefika Ngorongoro zaidi ya mara 30 lakini kinachoshangaza kila mwaka anaotembelea eneo hilo anashuhudia ng’ombe kuongezeka kuliko wanyama ambapo kipindi hicho walionekana kwa urahisi katika maeneo mbalimbali.

“Hali hii inatisha na serikali isipochukua hatua miaka kumi ijayo watalii watakuwa wanakuja kuangalia ng’ombe na mbuzi badala ya kuja kuona wanyama pori,tunaiomba serikali ifanye utaratibu mahsusi kuhakikisha kuwa hifadhi yetu inalindwa”,alisema Mzee Salim.

Kwa upande wake mwandishi wa habari wa masuala ya malengo ya milenia bwana Frank Soteri aliipongeza serikali kwa uamuzi wa kuwahamisha kwa hiyari wananchi wanaoishi katika tarafa ya Ngorongoro ili waweze kupata haki zao za msingi za binadamu ikiwemo uhuru wa kuishi kwani suala la wanyama kushambulia binadamu halikubaliki.

“Hao wanaotupinga tusihamishe watu kwa hiyari kutoka ndani ya hifadhi ndio wanaosisitiza kila mwananchi awe na umeme,maji,elimu na afya bora,sasa hiki kinachofanywa na serikali kwa kuhamisha watu kwa hiyari ni utekelezaji wa malengo yale yale ambayo dunia inahitaji”, alisema bwana Soteri.

Waandishi hao wamepata nafasi ya kufika katika kijiji cha Msomera kilichopo wilaya ya Handeni Mkoani Tanga na kushuhudia namna serikali ilivyowekeza kwa kujenga miundo mbinu mbalimbali katika eneo hilo.

No comments