Breaking News

SERIKALI KUWEKA MKAZO KUKUZA TASNIA YA UFUGAJI WA KUKU

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa ujio wa Mkutano wa Jukwaa la Tasnia ya Kuku na ndege wafugwao kwa Nchi za Kusini mwa Afrika unadhihirisha namna Tanzania chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia ilivyokuwa na mahusiano mazuri ambayo yamefungua milango katika sekta mbalimbali ikiwemo ya tasnia ya kuku na ndege wafugwao.

Amesema hayo leo Oktoba 16, 2024 jijini Dar es salaam wakati akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdory Mpango katika ufunguzi wa mkutano huo.

Ametaja faida za ufugaji kuku na ndege wafugwao kuwa ni pamoja na kuchangia usalama wa chakula na kuongeza pato la Taifa kikanda na kimataifa.

Amesema kuwa asilimia 55 ya kaya nchini na katika nchi mbalimbali ni ufugaji unaofanywa zaidi na wanawake na vijana na kuwa Tanzania ina kuku milioni 103.1 wakiwemo kuku wa asili na kisasa.

Kupitia Jukwaa hilo, Dkt. Biteko ameiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuanzisha mashamba ya kuku wazazi kwa ajili ya kuzalisha vifaranga, kuanzisha vituo vya kisasa, maabara pamoja na kuwekeza katika machinjio ya kisasa ya kuku.

Dkt. Biteko ametoa maagizo mengine ikiwemo “ Wizara iweke pia mfumo wa mnyororo baridi wa usambazaji wa kuku, iwekeze pia katika vizimba, chakula cha kuku na ianzishe viwanda vya kusindika vyakula vya kuku ili vipatikane ndani ya nchi na sio kutumia fedha za kigeni kuagiza nje,” 

Ametoa wito kwa wadau wote wa ufugaji wa kuku kuendelea kushirikiana na Serikali kutekeleza majukumu yao kwa kuwa Serikali imetoa fursa kwa kila mmoja kuweza kujishughukisha na kujiongezea kipato.

Dkt. Biteko ameikaribisha sekta binafsi kushiriki katika tasnia hiyo ili kusaidia kukuza uchumi wa nchi huku akiwataka watafiti kushirikiana na Serikali.
Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa kufanyika kwa mkutano huo ni matokeo ya mkutano wa AGRA uliofanyika Dar es alaam na kuongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia ambapo AGRA walielezwa juu ya kuipa kipaumbele sekta ya ufugaji wa kuku kwa kuwa nchini Tanzania familia nyingi zinafuga kuku

“Tunawashukuru AGRA na Food Alliance kwa kutukubalia na ndio maana leo jukwaa la kwanza limefanyika hapa Tanzania na kutoa fursa kwa wafugaji wetu kujifunza na kujenga mahusiano,” amesema Mhe. Ulega.

Amebainisha kuwa takwimu zinaonesha kuwa ifikapo 2030 kuku watachangia asalimia 41 ya protini na kuwa watafiti nchini washirikiane na Serikali wanapotoa matokeo ili kutoleta taharuki kwa jamii kupitia matokeo ya tafiti zao.

“Hivi karibuni watafiti walifanya utafiti kwa kutumia sampuli chache juu ya ulishaji wa kuku wanaofugwa na akina mama na vijana tafiti ile ilileta taharuki, kupitia Jukwaa hili nitumie fursa hii kuwaambia watafiti washirikiane na Wizara ili kutotoa taarifa za taharuki kwa jamii na kuwa Serikali inaweza kudhibiti wafugaji wasiofuata taratibu hivyo tusiharibu jitihada zinazofanywa na kukuza tasnia hii,” amesema Mhe. Ulega.

“Tunawaheshimu na kuthamini kazi zao ila tuone wanapofanya tafiti na kupeleka kwa jamii tuwe na mkakati wa pamoja wa kufikisha tafiti hizo kwa jamii,” amesisitiza Mhe. Ulega.
Naye, Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia na Mwenyekiti wa Bodi ya Muungano wa Mapinduzi ya Kijani barani Afrika (AGRA), Mhe. Dkt. Hailemariam Dessalegn, amesema kuwa fursa muhimu zilizopo kupitia ufugaji wa kuku ni chanzo cha protini, soko la uhakika na ajira kwa vijana na ka kushiriki katika mnyororo wa thamani.

“Jukwaa hili linatoa fursa ya kujifunza faida na changamoto katika tasnia hii na kuongeza ushirikiano. Kukuza tasnia hii katika nchi yetu inahitaji majukwaa kama haya na inahitaji utayari wa wadau mbalimbali kwa kuwa wana uwezo wa kuwekeza ili kukuza tasnia hii,” amesema Mhe. Dessalegn.


No comments