Breaking News

GST YAITANGAZA HUDUMA YA MAABARA YA GEOTECHNICAL

Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) inaendelea kutangaza huduma zinazotolewa na taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na huduma za Maabara ya _Geotechnical_ inayopima uimara na uwezo wa sampuli za miamba, udongo na kokoto zitakazotumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo majengo ya aina zote, madaraja, barabara, mabwawa na migodi (open pit & underground).

Elimu hiyo inaendelea kutokewa katika Maonesho ya Saba ya Kitaifa ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya Bombambili Mkoani Geita.
Akizungumza katika Maonesho hayo Meneja ya Masoko kutoka GST, Priscus Bernard amesema, maabara ya GST ina vifaa vya kisasa vinavyopima sampuli kwa ustadi na viwango vya juu ili kumwezesha mwananchi kujenga katika ubora wa kudumu. 

Aidha, Priscus amesema huduma hiyo inaweza kumsaidia mchimbaji wa madini katika mgodi mbalimbali kufanya uchimbaji salama kwa kupima uwezo wa miamba itakayotumika kama nguzo migodini

Pia, Priscus amesema huduma ya maabara kutoka GST inaweza kuwasaidia walipuzi migodini kupima uwezo wa miamba kabla ya kulipua maeneo husika.

Maonesho ya Kitaifa ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini yanayoendelea Mkoani Geita yamebebwa na Kauli mbiu isemayo "Matumizi ya Teknolojia Sahihi na Nishati Safi kwa Maendeleo Endelevu".




No comments