Breaking News

UTENDAJI KAZI MAHIRI UWE KIPIMO CHA KUITANGAZA SEKTA YA NISHATI NCHINI - KAMISHNA LUOGA

📌 Apongeza Wataalam Wizara ya Nishati/Taasisi kwa kutoa huduma bora kwa wananchi SABASABA

📌 Asema ni sehemu sahihi ya kupata mrejesho wa utendaji kazi

📌 Ataka wadau wa Nishati Safi ya Kupikia kuwa na kanzidata

Dar es salaam:
Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga amewataka Wataalam katika Wizara ya Nishati na Taasisi zake kujikita katika kufanya kazi kwa kasi, umakini na bidii ili kuwafikishia wananchi nishati ya uhakika na kwamba hicho ndicho kiwe kipimo kikuu cha kutangaza kazi za Wizara kwa wananchi.

Kamishna Luoga amesema hayo wakati alipotembea Banda la Wizara ya Nishati na Taasisi zake katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara (SABASABA) yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
“Sisi Wizara ya Nishati tumejipa changamoto ya kuongeza bidii zaidi ya kufanya kazi na kutoa huduma bora kwani  Watanzania wanachotaka ni nishati ya kutosha ikiwemo ya umeme  bila kuwa na usumbufu wowote.” Amesema Mha.Luoga 

Ameeleza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuhakikisha kuwa inatoa fedha za kutekeleza miradi ya uzalishaji, usafirishaji, usambazaji umeme pamoja na miradi mingine ya Nishati akitolea mfano mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) unaotekelezwa kwa kiasi cha shilingi trilioni 6.5 ambao sasa umefikia asilimia 98.

Ametaja baadhi ya miradi mingine ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa  kuwa ni pamoja na ya usafirishaji umeme itakayounganisha Mkoa wa Katavi na Kigoma kwenye gridi ya Taifa ambayo ni mradi wa usafirishaji umeme kutoka Tabora hadi Katavi na Tabora hadi Kigoma pamoja na miradi ya kuboresha upatikanaji umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Kuhusu Maonesho ya SABASABA amesema “nimetembelea mabanda ya Maonesho ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake na kuona jinsi Wataalam wanavyohudumia wananchi kwa umahiri na kutoa huduma mbalimbali ikiwemo za kuunganisha umeme kupitia mfumo wa Nikonekt,  kuonesha wananchi kwa vitendo matumizi ya nishati safi ya kupikia na kutatua changamoto mbalimbali ambazo wananchi wanaziwasilisha.”

Ameeleza kuwa, Maonesho hayo ni muhimu kwani Serikali inapata wasaa wa kutoa taarifa za utekelezaji wa majukumu yake kwa wananchi na pia kupata mrejesho wa huduma inazotoa, suala ambalo ni muhimu katika kupima utendaji kazi.

Kuhusu utekelezaji wa ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia, Mha. Luoga amewaasa wananchi kutumia nishati iliyosafi ambapo amewahamasisha kutumia majiko ya umeme yanayouzwa kwa gharama nafuu, yanatumia umeme kidogo na kupika chakula kwa muda mfupi ikiwa ni matokeo ya teknolojia mpya iliyobuniwa na TANESCO kwa kushirikiana na kampuni ya TaTEDO na SESCOM.

Aidha, amewataka wadau wa nishati hiyo kuhakikisha kuwa wanakuwa na kanzidata itakayojumuisha masuala mbalimbali ikiwemo idadi ya wananchi wanaotumia nishati iliyosafi, matumizi yake n.k ambayo itatumika kama moja ya njia za kujitathmini katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia na kuchukua hatua stahiki zitakazowezesha mkakati huo kutekelezwa kwa ufanisi.



No comments