Breaking News

WAZIRI MKUU ATAKA MIPANGO ENDELEVU YA UTAFUTAJI TEKNOLOJIA SEKTA YA MADINI.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Madini iendelee kushirikiana na wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi katika kutafuta teknolojia mbalimbali za uongezaji thamani madini.

Amesema kuwa kufanya hivyo kutawezesha madini yanayopatikana nchini kutumika katika kuzalisha bidhaa ambazo zinahitajika duniani kote kutokana na kuongezeka kwa mahitaji na kuendelea kuongezeka kwa idadi ya watu duniani. 

Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Juni 27, 2024) wakati alipofunga wiki ya madini iliyoambatana na Kongamano la Wachimbaji Madini, Mkutano Mkuu wa FEMATA pamoja na Maonesho ya Madini na Vifaa vya Uchimbaji iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, Jijini Dodoma.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa rai kwa Wafanyabiashara, Taasisi za Elimu, Taasisi za Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Madini kuendelea kuweka mikakati ya kuwezesha uwekezaji wa ndani wa teknolojia mbalimbali nchini zitakazowezesha upatikanaji wa malighafi zinazohitajika na migodi na shughuli nyingine za madini.

“Kwa kuwa teknolojia duniani inazidi kukua kwa kasi wadau wa madini waongeze na kuimarisha mtandao na wachimbaji  wa kikanda na kimataifa. “Kwakujifungia ndani peke yetu hatutapata suluhisho lachangamoto tulizonazo bali tutachelewesha maendeleo yetu”
Amesema kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto, kero na adha zinazowakabili wawekezaji na wachimbaji wa madini pamoja na kuhakikisha wanapata masoko ya uhakika ya kuuza madini pamoja na kuendelea kuwawezesha wawekezaji wadogo katika Sekta ya Madini kwa kuwaunganisha na Taasisi za Fedha nchini ili waweze kupewa mikopo.

“Katika hili  nitoe wito kwa taasisi za Fedha nchini kukaa na FEMATA, wapeni miongozo na elimu ya mitaji ili waweze kuitumia katika kuzipa thamani kazi zao ili ziwe na tija”

Kwa Upande wake, Waziri wa Madini Anthony Mavunde amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa nguvu sekta ya madini ili iendelee kutoa mchango katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania

Amesema kuwa Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Madini kutoka shilingi bilioni 89 hadi kufikia shilingi bilioni 231. “Mipango yetu ni  kuendelea kufanya tafiti za kina ili kubaini sehemu yalipo madini, pia tumepanga kununua helkopta ya kisasa ya itakayobaini kilichopo hadi urefu wa kilomita moja chini ya ardhi pamoja na  kujenga maabara kubwa ya kisasa katika sekta ya madini”
Pia Mheshimiwa Mavunde amesema Wizara inaendelea kutekeleza mpango wa kufuta leseni na maombi kwa wawekezaji waliochukua maeneo makubwa ya uchimbaji madini lakini hawayaendelezi na kuwapatia Watanzania wenye nia ya kuchimba ili wanufaike na rasilimali hiyo muhimu.

Naye, Rais wa Chama cha Wachimbaji Wadogo Tanzania (FEMATA) John Wambura amesema kuwa Tanzania inafursa ya kuwa na Soko la madini Afika kwa kuwa ina kila sifa ya kufikia hapo na hii ni kutokana na juhudi zilizofanywa na Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan

Aidha amesema kuwa katika mwaka 2024-2025 FEMATA imepanga kuendelea kuwaomgezea ujuzi na maarifa wachimbaji wadogo wengi zaidi pamoja na kuwaunganisha na Serikali ili kusaidia kuongeza vipato vyao na Taifa kwa ujumla “Pia tumeandaa vitambulisho ili tuweze kutambua kila mchimbaji alipo na anafanya nini”