Breaking News

WAZIRI MAJALIWA AZINDUA RIPOTI ZA KIDEMOGRAFIA, KIJAMII, KIUCHUMI NA MAZINGIRA ZINAZOTOKANA NA SENSA YA WATU NA MAKAZI YA 2022

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa (Mb) amezindua rasmi Ripoti za Kidemografia, Kijamii, Kiuchumi na Mazingira zinazotokana na Sensa ya Watu na Makazi na Sensa ya Majengo ya Mwaka 2022.

Amezindua ripoti hizo leo Juni 22, 2024 katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Uzinduzi huo umewakutanisha wadau mbalimbali na viongozi akiwemo, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, na Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa.

"Ni siku muhimu kwa kuwa leo tutashuhudia uzinduzi wa ripoti za Kidemografia, Kijamii, Kiuchumi na Mazingira zilizotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 Chapisho namba nne.

"Pamoja na ripoti ya kina iliyotokana na taarifa zilizokusanywa katika Sensa ya Majengo Nchini mwaka 2022.

Waziri Mkuu amesema, ripoti inayohusu majengo yote ni ya kwanza kutolewa nchini tangu kuasisiwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964.

Akizungumzia kuhusu umuhimu wa matokeo ya taarifa zilizokusanywa katika sensa zote tatu mwaka 2022, Waziri Mkuu amebainisha kuwa,

"Matokeo haya ni muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu kutokana na matumizi yake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba ripoti za matokeo ya Sensa zitakazozinduliwa hivi punde zinatupa fursa muhimu kama nchi kuendelea kutambua kwa kina zaidi hali zetu kidemografia, kiuchumi, kijamii na mazingira pamoja na hali ya makazi."
Pia, amefafanua kuwa, baadhi ya matokeo muhimu katika ripoti za takwimu za msingi zimedhihirisha matokeo chanya ya utekelezaji wa mipango ya kimkakati inayofanywa na Serikali zote mbili katika sekta mbalimbali.

"Matokeo yameonesha kuwa tumepiga hatua kubwa katika sekta ya elimu. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, kiwango cha kujua kusoma na kuandika kwa watu wenye umri wa miaka 15 na kuendelea kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kimeongezeka hadi asilimia 83.0 mwaka 2022 kutoka asilimia 78.1 ilivyokuwa mwaka 2012.

"Kwa upande wa sekta ya nishati, matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kupikia yameongezeka hapa nchini ambapo, kaya zinazotumia umeme kwa ajili ya kupikia zimeongezeka kutoka asilimia 1.6 mwaka 2012 hadi asilimia 4.3 mwaka 2022 na Gesi kutoka asilimia 0.9 mwaka 2012 hadi asilimia 9.4 mwaka 2022."

Amesema, idadi ya kaya zinazotumia kuni aiili va kunikia zimepungua kutoka asilimia 68.5 Haya ni mafanikio makubwa katika uhifadhi na utunzaji wa mazingira. Sote tunafahamu kuhusu madhara yanayosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa ambayo ni pamoja na kuchangia ongezeko la athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, athari kwa afya za watumiaji pamoja na kuleta athari nyingine za kiuchumi katika jamii."

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema sekta ya maji na mazingira imeendelea kufanya vizuri ambapo matokeo ya Sensa yanaonesha kuwa asilimia 70.1 ya kaya zote zinatumia maji kutoka katika vyanzo vilivyoboreshwa.

"Asilimia 60.2 ya kaya zinatumia vyoo vilivyoboreshwa. Hili ni jambo la kujivunia sana.hayo ni baadhi tu ya matokeo muhimu ya ripoti hizo.

"Nimetaarifiwa kuwa ripoti zimesheheni taarifa za kina zaidi na zimebainisha kwa kina ya hali ya nchi yetu katika nyanja za kijamii, kiuchumi na mazingira ikiwa ni pamoja na hali ya majengo ya makazi na yasiyo ya makazi."
"Kama mnavyofahamu, hivi sasa nchi yetu inaendelea па mchakato wa kutathmini utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025 ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050.

"Matokeo haya na mengine ya Sensa ya Watu na Makazi, Sensa ya Majengo na Sensa ya Anwani za Makazi ya Mwaka 2022 yana nafasi ya kipekee katika kusaidia tathmini na kufanya maandalizi thabiti ya Dira hizo kwa manufaa mapana ya Watanzania wote."

Amesema, Serikali katika pande zote mbili za Muungano imekuwa ikisisitiza kuhusu kuimarisha masuala ya ufuatiliaji na tathmini.

"Hivyo basi, matokeo ya Sensa yataendelea kutumika katika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya nchi yetu ya muda mfupi, muda wa kati, na muda mrefu kama vile Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Mwaka 2021/2022 -2025/2026 na Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar wa Mwaka 2021/2022- 2025/2026.

"Nimefarijika sana kwa kuwa matokeo hayo yametumika kikamilifu katika kutayarisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/2025, kwa msingi huo, sina shaka Bajeti imegusa uhalisia wa mahitaji ya wananchi katika nyanja zote."

Waziri Mkuu amesema, matokeo ya takwimu za Sensa yaliwezesha Serikali kuchukua hatua za haraka na madhubuti katika kubainisha kiwango cha madhara yaliyotokana na majanga ya maporomoko ya udongo yaliyotokea katika Wilaya ya Hanang' mkoani Manyara na mafuriko katika Wilaya ya Rufiji iliyoko mkoani Pwani.

Amesema, taarifa ziliwezesha kuandaa mikakati ya kuwafariji wananchi walioathirika. "Mafanikio hayo yote yametokana na uwepo wa matokeo ya takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ambazo zimeunganishwa na takwimu za Sensa ya Majengo na Anwani za Makazi.

Kwa maneno mengine, ripoti hizi zina mchango mkubwa katika kutunga na kuhuisha sera mbalimbali zinazohusiana na masuala ya ustawi wa wananchi ikiwemo uwezeshaji wa wananchi kiuchumi."

Amesema, kutokana na umuhimu huo, ni matarajio ya Serikali kuona mipango yetu katika ngazi zote za utawala ikiwemo ya kibajeti inazingatia uhalisia unaotokana na matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi na Sensa ya Majengo ya Mwaka 2022.

"Nasisitiza jambo hili kwa kuwa tukifanya hivyo sio tu itatuwezesha kutumia rasilimali tulizonazo kwa ufanisi itatuwezesha kuona au kupata thamani halisi ya takwimu zitokanazo na Sensa ambazo ni hazina kubwa kwetu kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali."
SENSA YA MAJENGO YA MWAKA 2022

Waziri Mkuu amesema, kwa mara ya kwanza, mwaka 2022 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilifanya Sensa ya Majengo sambamba na Sensa ya Watu na Makazi na Sensa ya Anwani za Makazi.

Amesema, Sensa hiyo, imeifanya Tanzania kuwa moja ya nchi chache Barani Afrika ambazo zimeweza kufanya mazoezi hayo makubwa ya Kitaifa kwa pamoja.

"Sina shaka mtakubaliana nami kuwa matokeo yaliyobainishwa katika Ripoti ya Takwimu za Msingi za Sensa ya Majengo ni muhimu sana kutokana na sababu zifuatazo.

"Kwanza, yatasaidia kuongeza ufanisi katika maeneo mbalimbali ya sekta ya nyumba ikiwa ni pamoja na kukusanya maduhuli ya Serikali hasa kodi za majengo kupitia mita namba za umeme zilizokusanywa wakati wa zoezi la Sensa ya Majengo,

"Pili, uhuishaji wa kanuni za mipangomiji Tanzania Bara hususan viwango vya kupanga ukubwa wa maeneo kwa matumizi ya ardhi na makundi ya matumizi na madaraja ya mat ya ardhi zote za mwaka 2024,

"Tatu, kuhuisha taarifa za umiliki, matumizi ya jengo, namba za simu za wamiliki na majira nukta ya majengo husika. Vilevile, kanzidata ya Sensa ya Majengo itatumika kuhuisha mfumo wa 'Integrated Land Management Information System' (ILMIS) kwa ajili ya kuimarisha ufuatiliaji na utekelezaji wa sera mbalimbali za sekta ya nyumba."

Waziri Mkuu amesema matokeo hayo, yatachagiza juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi.

"Kama mtakumbuka nchi yetu haikuwa na takwimu za uhakika za majengo, lakini kupitia Sensa ya Majengo tumeweza kubaini idadi ya majengo yote nchini.

"Kwa mujibu wa takwimu zilizopo nchi yetu ina majengo milioni 14.3. Kati ya hayo, majengo milioni 13.9 yapo Tanzania Bara na takribani majengo laki 4 yapo Zanzibar.

Aidha asilimia 94.4 ya majengo yote siyo ya ghorofa. Isitoshe, majengo tisa kati ya kumi ni kwa ajili ya makazi na asilimia 3.4 ya majengo ni ya makazi na biashara."

SENSA YA ANWANI ZA MAKAZI YA MWAKA 2022

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema matokeo ya Sensa zote tatu, yaani Sensa ya Watu na Makazi, Sensa ya Majengo na Sensa ya Anwani za Makazi yamewezesha Mfumo wa Anwani za Makazi.

Mfumo huo umeweza kutoa barua za utambulisho wa mkazi kidijitali, kurahisisha utoaji wa anwani za makazi katika majengo mapya yanayoendelea kujengwa nchini.

Pia, kuwezesha taasisi za Serikali kutumia taarifa za Anwani za Makazi, kufanya uhakiki na kuboresha taarifa zilizokusanywa wakati wa operesheni Anwani za Makazi pamoja na kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa kidijitali.

"Sina shaka nyote mtakubaliana nami kuwa matokeo ya Sensa zote tatu, Sensa ya Watu na Makazi, Sensa ya Majengo na Sensa ya Anwani za Makazi yamekuwa na tija sana katika kupanga, kupima na kutathmini utekelezaji wa sera na mipango mbalimbali ya maendeleo ya nchi yetu tuliyojiwekea."

MCHANGO WA UZOEFU

Waziri Mkuu amesema, kupitia utekelezaji wa Sensa ya kidijitali ya Watu na Makazi, Sensa ya Majengo na Sensa ya Anwani za Makazi ya Mwaka 2022, Tanzania imetoa mchango wa uzoefu wake katika kufanikisha sensa za nchi nyingine Kikanda na Kimataifa.

"Ninawapongeza sana wataalamu wetu kwa kuwa ninafahamu, jirani zetu wakiwemo Uganda walifika nchini kwetu kujifunza namna tulivyofanikisha Sensa kwa weledi na wakatualika kwenda kushauri namna bora ya utekelezaji wa Sensa yao ya kidijitali iliyofanyika mwezi Mei, 2024.

"Ninawapongeza sana kwa utaratibu huo mzuri wa kubadilishana uzoefu kwa wataalamu kutoka nchi za jirani."

Amesema, Kimataifa Tanzania imeshaalikwa mara kadhaa na Umoja wa Mataifa kutoa uzoefu wake katika utekelezaji wa Sensa ya kidijitali katika kuzisaidia nchi nyingine ambazo zilikuwa zinajiandaa kufanya Sensa zao.

Ni katika Mzunguko wa miaka ya 2020 ya Umoja wa Mataifa wa Kufanya Sensa, ambao ulianza mwaka 2015 na utaisha mwaka 2024.

Aidha, amesema Tanzania ni miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya Kitaalamu ya Umoja wa Mataifa inayohuisha Kanuni na Mapendekezo ya Umoja wa Mataifa wa kufanya Sensa.

"Kanuni na Mapendekezo hayo yatawasilishwa kwenye Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Takwimu na baadaye kwenye Kikao cha Umoja wa Mataifa cha Wakuu wa Nchi na Serikali kwa ajili ya kuridhiwa.

"Licha ya hayo, Sensa hii imetoa fursa ya ajira kwa wataalamu wetu wa teknolojia ya habari katika Bara la Afrika kwa nchi ambazo zinaendelea na utekelezaji wa Sensa zao za kidijitali kama vile Namibia, Nigeria, Zambia na Uganda.

"Mambo yote hayo yamewezekana kutokana na utashi mkubwa wa siasa wa Viongozi wakuu katika masuala ya takwimu.

"Mambo yote hayo yamewezekana kutokana na utashi mkubwa wa siasa wa Viongozi wetu wakuu katika masuala ya takwimu.

"Viongozi wetu wamekuwa tayari wakati wote kutuwezesha upande wa rasilimali, pamoja na kutoa miongozo makini ambayo imetufikisha katika hatua hii ya mafanikio makubwa tunayojivunia leo ndani ya nchi yetu, kikanda na kimataifa."

UTEKELEZAJI WA MWONGOZO

Waziri Mkuu akizungumzia kuhusu utekelezaji wa Mwongozo wa Kitaifa wa Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi amesema, kwa sasa tupo katika Awamu ya Tatu na ya mwisho ya utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.

"Kazi zinazoendelea zimeelezwa kwa ufasaha ikiwemo utekelezaji wa Mwongozo wa Kitaifa wa Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.

"Sina shaka sote tumeshuhudia namna ambavyo Serikali inatekeleza Mwongozo huo ambao ni maagizo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyoyatoa wakati alipokuwa akizindua matokeo ya mwanzo ya Sensa mwezi Oktoba, 2022.

"Kama mtakumbuka, Mheshimiwa Rais, alisisitiza kuhusu usambazaji, uhamasishaji na mafunzo ya matumizi ya matokeo ya Sensa ili kuhakikisha yanatumika kikamilifu katika mipango ya maendeleo katika ngazi zote za utawala."

MAENEO YA MSISITIZO

Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Mkuu amewaagiza watendaji wote wanaohusika na sera na mipango katika Serikali Kuu, tawala za mikoa na Serikali za mitaa wahakikishe kuwa mipango maendeleo mbalimbali na maamuzi yote yanayohusu ikiwemo utoaji wa kwa wananchi matokeo hayo ya Sensa.

"Serikali ingependa kuona matokeo ya Sensa yanatumika kikamilifu katika kubaini na kutatua changamoto zinazoikabili jamii yetu kwa namna ambayo ni endelevu.

"Nirudie kusisitiza kuhusu umuhimu wa matumizi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi katika ngazi zote za utawala wakati tunapopanga mipango maendeleo ya wananchi."

Jambo lingine, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameagiza matumizi ya matokeo hayo ni ya kila Mtanzania kwa kuwa ni mali ya umma. Hivyo, mkakati wa uelimishaji umma katika maeneo mbalimbali uendelezwe.

"Maafisa masuuli wote wahakikishe utekelezaji wa vipaumbele vilivyoanishwa kwenye bajeti uzingatie uhalisia wa takwimu zilizobainishwa katika Sensa.

"Ninatambua bajeti imezingatia sensa hivyo ninasisitiza utekelezaji wake pia ujikite katika uhalisia wa takwimu zilizopo.

"Nitoe wito kwa asasi za kiraia, mashirika ya Kimataifa, mashirika yasiyo ya Serikali na sekta binafsi kwa ujumla kutumia taarifa za matokeo ya Sensa katika upangaji wa mikakati yao.

"Hii itawezesha kuongeza kasi ya usambazaji huduma kwa wananchi badala ya kurundika afua zote katika eneo moja kuzingatia idadi ya wahitaji."

Vilevile, Waziri Mkuu amewataka wanazuoni, wanataaluma na watafiti watumie Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 katika kufanya shughuli zao za kitaaluma.

"Taarifa zilizopo zimegusa maeneo muhimu ambayo yatakuwa na mchango mkubwa katika uandishi wa makala, ufundishaji na ujifunzaji na uthibitishaji wa nadharia za kitaaluma."