Breaking News

NGORONGORO YASISITIZA KUENDELEA KUHAMISHA WATU KWA HIYARI


Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imesema itaendelea kuelimisha na kuhamisha wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi ya eneo hilo kwa hiyari na haitotishika na kelele za baadhi ya vikundi vya watu wanaowatumia wananchi hao kupata kipato kupitia baadhi ya mashirika duniani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha mwishoni mwa wiki kaimu meneja wa uhusiano kwa umma  wa mamlaka hiyo Hamis Dambaya amesema mpaka sasa zoezi linakwenda vizuri na wananchi wengi wanataka kutoka katika eneo hilo ambapo serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa nyumba na miundo mbinu mingine ili kuhakikisha wananchi hao wanahama.

Dambaya amesema kazi ya ujenzi wa nyumba inayofanywa na Jeshi la Kujenga Taifa katika Kijiji cha Msomera inakwenda vizuri na takribani kila siku nyumba zinakamilika huku zoezi la kuelimisha wananchi kuondoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro nalo likiendelea kufanyika ili kuhakikisha kila mwananchi anayetaka kuhama anaondoka.

“Zoezi letu tunalifanya kwa uangalifu mkubwa katika kuhakikisha kuwa hakuna mtu ambaye anahamia kwa sasa kutoka sehemu nyingine nchini au nchi Jirani anahamishwa hasa ikizingatiwa kwamba wananchi wengi wa Tanzania wanaona kwamba zoezi hilo kwa wananchi hao ni fursa kubwa ya kukuza uchumi na maisha yao kulinganisha na maisha ndani ya hifadhi na ikibainika kuna mtu ameghushi makazi na kuhamishwa atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi,”alisema Dambaya.

Kuhusu madai ya kukiukwa kwa haki za binadamu katika eneo hilo la hifadhi ya Ngorongoro bwana Dambaya amesema mamlaka hiyo inatambua wazi kuwa hoja hiyo inatolewa na baadhi ya watu ambao wananufaika kupitia mgongo wa wananchi hao kwa kuidanganya dunia kuwa kuna ukiukwaji wa haki za binadamu ili wapate fedha.

“Kwa muda mrefu jamii ya watu wanaoishi ndani ya hifadhi wamekuwa wakitumika na baadhi ya mashirika na waandishi wa habari kama chanzo cha kupata fedha kutoka kwa baadhi ya mataifa na mashirika ya nje hivyo wanaumia wanapoona wananchi hao wanahama kwa hiyari kwani wanatambua huko mbele watakosa chanzo cha kujipatia fedha,”alisema bwana Dambaya.

Amesema Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro  haijawahi kumuondoa mtu kwa nguvu kutoka ndani ya hifadhi na ndio maana hata baadhi ya taasisi zinazotoa madai hayo zimekuwa zikipiga kelele zikiwa nje ya Tanzania na wengi wao hawana upeo wowote kuhusu maisha ya wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi.

Serikali ya Tanzania inaendelea kuwahamisha wananchi kutoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kuimarisha maisha yao hasa kutokana na idadi ya watu na wanyama  kuongezeka na hivyo kuathiri uhai wa wananchi hao.

Itakumbukwa kwamba wakati hifadhi hiyo inaanzishwa mwaka 1959 ilikuwa na wakazi elfu nane tu ambapo mpaka kufikia sasa hifadhi hiyo ina zaidi ya watu laki moja jambo ambalo limewafanya waishi maishi magumu na kukosa maeneo ya kufanyia shughuli zao za kimaendeleo.

Tangu kuanza kwa zoezi hilo baadhi ya taasisi ambazo zimekuwa zikiwatumia jamii ya wamasai wanaoishi ndani ya hifadhi kama sehemu ya kujipatia fedha zimekasirishwa na zoezi hilo na zimekuwa zikizunguka nchi mbalimbali duniani kuomba msaada wa kifedha ili kudhoofisha uhamaji huo unaofanyika kwa hiyari. 

No comments