Breaking News

BANDARI YAANZA KUPOKEA MELI KUBWA ZA MIZIGO

Picha na mtandao

Na Mwandishi Wetu, Dar 
Bandari ya Dar es Salaam imeweka rekodi kwa kupokea meli kubwa ya mizigo yenye urefu wa mita 294.1 tofauti na meli ambazo imewahi kuzipokea hapo awali kwani meli ya mwisho kupokelewa ilikuwa na urefu wa mita 267 hatua inayotafsiriwa kama sehemu ya mafanikio ya uwekezaji mkubwa  uliofanywa katika bandari hiyo..

Akizungumza  na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili kwa meli hiyo kwenye  Bandari ya Dar es Salaam jana, Meneja Mizigo Mchanganyiko  wa Banadari ya Dar es Salaam,  Bw.  Abed Gallus alisema kuwa meli ya (MSC ADU -V) imekuwa meli  ya kwanza kubwa  kuwasili katika bandari hiyo kwani ina uwezo wa kubeba makontena 4000.

"Hii ni historia kwetu  kwani hapo awali tulikuwa tunapokea meli zenye urefu wa mita 267  lakini sasa tunauwezo wa kupokea meli zenye uwezo ukubwa wa  mita 305  haya ni mafanikio makubwa kwetu kama Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA),” alisema Bw Abed.

Bw Abed alisema uwekezaji mkubwa  wa miundombinu uliofanywa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia TPA katika  Bandari ya  Dar es Salaam umechangia  kiasi kikubwa kuongezeka ufanisi wa kiutendaji  ambapo awali  likuwa  na kina  cha wastani wa mita  8 mpaka 12.7 lakini  sasa kimeongezwa na  kufikia mita  14.5 na kuwa na uwezo wa kupokea  meli yenye urefu  wa mita zaidi ya 305.

“Tunazipongeza  hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya ambayo imewekeza vya kutosha katika  Bandari ya Dar es Salaam ikiwemo kuongeza kina na vitendea kazi katika bandari yetu na hivyo  kutoa matokeo chanya  ikiwemo kuanza kupokea meli kubwa,” alisema.

Aidha , Bw Abed alisema moja ya faida ya kubwa kupokea meli kubwa za mizigo ni  kupungua kwa gharama za kusafirisha mizigo ambapo italeta unafuu kwa wafanyabiashara na wasafirishaji wa mizigo  sambamba na  kuchochea ushindani wa bandari zilizopo ukanda wa Afrika mashariki na kati.

"Kumekuwa na ufanisi mkubwa ikiwemo kuhakikisha upakuaji wa mizigo unafanyika kwa haraka zaidi kwani  ndani ya masaa 24 tuna uwezo wa kupakua wastani wa makontena 800 hivyo tunatarajia ndani ya siku tano meli hii itakuwa imeshapakia na kuondoka katika bandari yetu," alisema Bw Abed.

Bw Abed alisema  kuwa   Bandari ya Dar es Salaam ni miongoni mwa bandari sita ambazo TPA inazisimamia na   kwa kuliona hilo Mamlaka imeendelea kuboresha bandari nyingine ili kutoa msaada kwa Bandari ya Dar es Salaam ambayo zaidi  ya asilimia 95 ya mizigo inapita katika bandari hiyo.  

"Tumendelea kuboresha miundombinu ya  bandari zetu ikiwemo pamoja na bandari ya Mtwara na Tanga  ambapo tayari tumeshanunua vifaa vya upakuaji mizigo  kwani hapo awali  Bandari ya Tanga, meli zilikuwa zinafungwa nje ya gati  lakini sasa hivi meli zinaingia kwenye gati. Maboresho haya yote ni juhudi za mamlaka kuhakikisha bandari hizo zinatoa msaada kwa Bandari ya Dar es salaam," alisema Bw Abed.

Katika kufanya kazi kiushindani sambamba na kujiimarisha kibiashara, TPA imeingia mikataba ya kiuendeshaji katika baadhi ya gati zake kwa Bandari ya Dar es salaam, kwa kufanya hivyo itaongeza ufanisi   na hivyo kufanya bandari  hiyo kuwa  kinara kwa uingizaji na usafirishaji wa mizigo kwa nchi nyingi zikiwemo za maziwa makubwa na kusini mwa jangwa la Sahara. 

No comments