Breaking News

TAKUKURU PWANI YAONGEZA MAPATO MACHINJIO MTAKUJA

Kaimu Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani Ally Sadiki akifafanua jambo katika mkutano na Waandishi wa Habari ofisini kwake, kibaha mkoani pwani.

Na Mwandishi Wetu Kibaha
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani imefanya uchambuzi wa mfumo wa ukusanyaji wa mapato yatokanayo na machinjio ya Mtakuja iliyopo Halmashauri ya Mji Kibaha.

Akizungumza na mwaandishi wa habari juu ya mambo mbalimbali yaliyojili katika kipindi cha Octoba hadi Disemba 2023, kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani Ally Sadiki amesema mara baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi walianza uchambuzi juu ya tuhuma hizo.

"Mara baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi tulianza kufanya Uchambuzi kuona kama kuna miaya ya rushwa katika ukusanyaji wa mapato na ushuru katika machinjio hayo na nini kilisababisha upotevu wa mapato na Halmashauri hivyo kupelekea kushindwa kufikia lengo la ukusanyaji mapato kama ilivyojiwekea" Alisema na kuongeza kuwa.

"Katika Uchambuzi huo tumebaini kwamba pamoja na kuwepo kwa mashine za kieletroniki za POS katika machinjio kumekua na taarifa zinazokinzana, kuwepo kwa miundombinu na ucheleshaji upelekwaji wa mapato benki". Alisema Kamanda Sadiki.

Alisema TAKUKURU imebaini pia kuwepo na uzembe katika zoezi la kusimamia idadi ya ng'ombe wanao chinjwa kwa siku pamoja na ukaguzi wa idadi ya ng'ombe waliopo eneo la kusibiri kuchinjwa.

Kamanda Sadiki aliongeza kuwa TAKUKURU pia imebaini kushindwa kufikiwa kwa malengo ya ukusanyaji wa mapato katika machinjio hayo kumechangiwa na uwepo kwa idadi ndogo ya watumishi walioajiriwa katika eneo husika.

Alisema kufatia hatua hiyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibaha Mji tayali ameshachukua hatua ya kuongeza watumishi eneo machinjio hayo ya Mtakuja hivyo kuimarisha ufuatiliaji na ukaguzi jambo lilopelekea kuongezeka kwa makusanyo ya mapato katika machinjio hayo kutoka Milioni 7.4 mwezi Oktoba 2023 hadi Milioni 9.6 mwezi Disemba.

Aidha Kamanda Sadiki iliongeza kuwa katika kipindi tajwa pia wamefanya chambuzi nyingine katika mifumo tano ikiwemo sekta ya Ardhi, Elimu, AMCOS na ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya serikali ili kupata tija ya mifumo imara usiyokwamisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Ameongeza TAKUKURU Mkoa wa Pwani pia wamefuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 23 yenye thamani ya Bilioni 6.3 katika sekta za Elimu, Maji, Afya na Ujenzi (Barabara), ambapo kati ya miradi hiyo ni mradi mmoja tu umeonekana kuwa na mapungufu na ufuatiliaji wake bado unaendelea kufatia kuwapa maelekezo ya kurekebisha kasoro hizo. 

Kamanda Sadiki aliongeza kuwa katika kipindi cha miezi mitatu imeweza kutoa elimu kwa umma kwa kufanya semina 19, mikutano ya hadhara 21, vipindi vya redio 9 kuimarisha klabu za wapinga rushwa 54, uandishi makala 4 na TAKUKURU Rafiki 6.

Aidha TAKUKURU Mkoa wa Pwani imefungua kesi mpya mbili Mahakamani ambapo kesi sita zimeamuliwa huku kesi nne watuhumiwa tayali wametiwa hatiani na kesi zingine sita zikiendelea Mahakamani. 

Alisema moja ya mikakati waliyojiwekea ni pamoja na kuendelea kufanya udhibiti wa mapato ya serikali na usimamizi wa rasilimali za umma ikiwa ji pamoja na udhibiti wa fedh zinazotolewa na serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo.