Breaking News

MATINYI: UCHUMI UMEKUWA KWA 5.2

Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi akizungumza na Wahariri pamoja na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya miaka mitatu ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Machi 24, 2024 katika Ukumbi wa Golden Jubilee, Dar es Salaam

Dar es salaam 
Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, amesema Tanzania imeendelea kuwa katika kundi la Nchi zenye uchumi wa pato la kati, ikimaanisha pato la wastani la kila Mwanachi kwa mwaka (GNI per capital) ambapo ingawa mwaka 2019 ilikuwa kiasi cha dola 1,080 (Tsh. 2,743,813) lakini mwaka 2022 ni dola 1,200 ( Tsh. 3,048,681).

Akiongea Jijini Dar es salaam leo, Matinyi amesema “Uchumi wa Tanzania umeendelea kukua licha ya athari kubwa za mlipuko wa UVIKO-19 duniani pamoja na vita za Urusi na Ukraine na pia huko Mashariki ya Kati, matatizo haya yaliutikisa uchumi wa Tanzania uliokuwa umefikia wastani wa ukuaji wa zaidi ya 7% na kuushusha hadi 4.2% mwaka 2020”.
“Hata hivyo, hivi sasa ukuaji umefikia 5.2% kutokana na uongozi thabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita, aidha Tanzania imeendelea kuwa katika kundi la Nchi zenye uchumi wa pato la kati, ikimaanisha pato la wastani la kila Mwanachi kwa mwaka (GNI per capital) ambapo ingawa mwaka 2019 ilikuwa kiasi cha dola 1,080 (Tsh. 2,743,813) lakini mwaka 2022 ni dola 1,200 ( Tsh. 3,048,681)”

“Serikali pia imeendelea kudhibiti mfumuko wa bei ambapo kwa sasa ni chini ya 4% - kiwango ambacho ni miongoni mwa viwango bora katika nchi za jumuiya za kikanda ambazo Tanzania ni mwanachama, kama Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)”

“Akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa toshelezi ambapo katika kipindi chote cha miaka mitatu hadi December 2023, Nchi ilikuwa na akiba inayotosha kuagiza bidhaa kutoka nje ya Nchi kwa miezi 4.5, ikiwa ni kiwango cha juu ya lengo la miezi 4, akiba hiyo ni sawa na dola za Marekani bilioni 5.4”