Breaking News

WAZIRI MAVUNDE ATOA MWELEKEO MPYA SEKTA YA MADINI

Serikali kupitia Wizara ya Madini imeweka mikakati ya kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa shughuli za utafiti wa madini nchini kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili kutoa taarifa sahihi za kijiolojia za madini na kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi sambamba na kuwawezesha wachimbaji wadogo.

Waziri wa Madini, Mhe Anthony Mavunde (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 11 Septemba 2024 Jijini Dodoma wakati akizungumza kwenye kikao cha pamoja kati ya wachimbaji wadogo chini ya mwamvuli wa FEMATA.

Amesema kuwa, ili kuongeza uwekezaji katika Sekta ya Madini, Wizara kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeweka mkakati wa kuhakikisha tafiti za kijiolojia zinafanyika katika maeneo yote nchini ifikapo mwaka 2030 ili kuwezesha wachimbaji wa madini wengi kuendesha shughuli zao bila kubahatisha na Serikali kuendelea kupata mapato ambayo yatawezesha kuimarisha sekta nyingine muhimu kama vile miundombinu, kilimo, nishati n.k.

“ Tafiti hizi zitawezesha kugundulika kwa madini ya kimkakati, malighafi kwa ajili ya kuzalisha mbolea hali itakayopelekea uwepo wa viwanda vya kuzalisha mbolea nchini, kuzalisha ajira mpya katika Sekta ya Madini na sekta nyingine na kupunguza migogoro kati ya wachimbaji wadogo wa madini na wachimbaji wakubwa wa madini,” amesema Mavunde.

Katika hatua nyingine, amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko alipokuwa Waziri wa Madini na kuongeza kuwa ataendeleza kazi nzuri iliyofanywa sambamba na kuomba ushirikiano kwa Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Madini ili kuhakikisha mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa unafikiwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025 huku wananchi wakiendelea kutajirika kutokana na uwekezaji katika Sekta ya Madini.

No comments