NBS YAWATAKA WAKUU WA MIKOA KUTUMIA TAKWIMU ZA MATOKEO YA SENSA
Dar es Salaam
OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imetoa mafunzo ya usambazaji na matumizi ya Matokeo ya Sensa kwa wakuu wa mikoa na makatibu Tawala wa mikoa.
Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyofanyika leo Agosti 31, 2023 jijini Dar es Salaam Kamishna Mkuu wa Sensa ya Watu na Kakazi 2022 Anne Makinda amesema mafunzo hayo yanahusu viashiria muhimu vya kiuchumi na mazingira kutokana na matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.
Makinda amewataka viongozi hao kupeleka elimu ya matokeo ya sensa kwa wananchi pamoja na kutumia matokeo hayo katika kupanga shughuli za maendeleo katika mikoa.
“Mnapaswa kutumia matokeo ya sensa katika kupanga shughuli za kimaendeleo katika mikoa yenu pamoja na kutoa elimu ya sensa kwa wananchi,” amesema Makinda akiwaeleza viongozi hao.
Ameeleza kwamba kuhesabu watu siyo mwisho, kazi kubwa iliyopo mbele yao na viongozi hao ni kupeleka elimu ya matokeo hayo ya sensa kwa wananchi ili waweze kuyaelewa na kuyatumia katika mipango hiyo ya maendeleo kwenye maeneo yao.
“Sisi wenyewe hatuwezi kumaliza nchi nzima kutoa elimu hii ya matokeo ya sensa, tunawategemea viongozi hawa na kamati zao za sensa kuyachukua haya na kuyapeleka kwa wananchi, bahati nzuri katika takwimu zetu zipo za hesabu ” ameongeza Makinda.
Amebainisha kwamba bidii, ubunifu na kujituma kwa wakuu wa mikoa na makatibu tawala kumefanya zoezi hilo la sensa kuendeshwa kwa urahisi na kufanikiwa kwa kiwango cha hali ya juu.
Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa amewashukuru wakuu wa mikoa kwa kutekeleza na kutoa ushirikiano katika kukamilisha zoezi la Sensa ya watu na makazi lililofanyika mwaka jana.
Dkt. Chuwa amesema matokeo ya sensa hiyo yameonesha kuwa umri wa Mtanzania kuishi umeongezeka kutoka miaka 44 hadi 65 na kwamba hizo ni juhudi ambazo zinafanywa na wakuu hao wa mikoa katika kumsaidia Rais kwenye utendaji kazi wake.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amesema lengo la mafunzo ni kutumia matokeo hayo ya sensa ya mwaka 2022 katika kupanga, kupima na kutahimini utekelezaji wa maendeleo.
“Lakini pia yataongeza uelewa wa kutosha wa matumizi wa matokeo ya sensa, sisi kama viongozi wa mikoa matokeo haya yatatusaidia katika kufanya maamuzi ya kitakwimu yanayoakisi hali halisi ya mahitaji ya wananchi,” amesema Telack na kuongeza,
“Kama tunavyofahamu suala la kupanga maendeleo ni shirikishi na linaanzia kwa wakuu wa mikoa kuanzia vijiji mpaka juu, hivyo kupitia mafunzo haya yatatuongezea ujuzi na uzoefu katika kutekeleza majukumu yetu ya kila siku,”.
No comments