Breaking News

EWURA TUNAYO MAFUTA YA KUTOSHA, YAVIFUNGIA VITUO VYA SITA

Dar Es Salaam
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewaondoa hofu Watanzania kuhusu hali ya upatikanaji wa mafuta nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dokta James Andilile amesema nchi ina mafuta ya kutosha na hakuna upungufu kama inavyoelezwa.

"EWURA imejiridhisha kuwa, nchi ina mafuta ya kutosha kwani kuna mafuta kwenye maghala na kuna mafuta mengine ambayo yako kwenye Meli zilizowasili bandarini zikisubiri nafasi ya kuingia kwenye gati na kushusha mafuta hayo," Alisema Dkt. Andilile.

Dkt. Andilile ametaja Meli zilizowasili kuwa ni Mt. Ellie Lady yenye takribani lita 58,069,544 za Dizeli kwa ajili ya matumizi ya hapa nchini ambayo iliwasili Agosti 29, 2023 ambapo imeanza kushusha mafuta Septemba 3, 2023 na inatarajia kumaliza kushusha Septemba 10, 2023.

Meli nyingine ni Mt. Emma Grace yenye takribani lita 17,234,333 za Petroli kwa ajli ya matumizi ya hapa nchini ambayo iliwasili Agosti 29, 2023 ambapo inatarajiwa kuanza kushusha mafuta Septemba 8, 2023 na kumaliza Septemba 12, 2023.

Ametaja Meli nyingine kuwa ni Mt. High Tide yenye takribani lita 22,302,452 za Petroli kwa ajili ya matumizi ya hapa nchini kwamba iliwasili Agosti 28, 2023 ambayo inatarajiwa kuanza kushusha mafuta Septemba 12, 2023 na kumaliza Septemba 16, 2023.

Hivyo Dkt. Andilile amesema kwa mafuta yaliyopo kwenye maghala n yale yaliyopo kwenye meli zilizowasili, nchi ina mafuta ya Petroli yatakayokidhi mahitaji ya siku 19, Dizeli kwa siku 18, mafuta ya Ndege kwa siku 36 na mafuta ya Taa kwa siku 58.

Kwamba pamoja na mafuta hayo, meli zitaendelea kuwasili hadi Oktoba 31, 2023 kulingana na mpangilio ulioainishwa katika zabuni za uingizaji wa mafuta kwa pamoja (BPS) zilizofanyika kufikia Agosti 31, 2023.

Akizungumzia kuhusu kwanini kuna upungufu wa mafuta baadhi ya mikoa, Dkt. Andilile amesema pamoja na kuwepo na mafuta, baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakichukua mafuta na kuchelewesha kufikisha vituoni huku wengine wakiwa na mafuta kwenye visima lakini hawauzi.

"Pia uchunguzi wa EWURA umebaini kuwa, kuna baadhi ya wauzaji wa mafuta kwa jumla (wholesalers) wameonekana wana mafuta kwenye maghala lakini hawauzi kwenye vituo. Mfano mmoja ni Kampuni ya GBP ambayo ina leseni ya jumla, lakini vituo vyake havina mafuta," amebainisha Dkt. Andilile na kuongeza,

"Kutokana na hatua hiyo, jana tuliamua kufunga kwa muda kituo kimoja cha GBP kilichopo mkoani Tabora na Mamlaka itavifunga vituo vingine iwapo havitauza mafuta. Iwapo hawatatoa utetezi unaojitosheleza kituo hicho kinaweza kufungiwa kwa kipindi cha miezi sita,".

Kuhusu hatua zilizochukuliwa kutokana na ufichaji wa mafuta, Dkt. Andilile amebeinisha kuwa EWURA imakamata wafanyabiashara 12 ambao wanajihusisha na tabia hiyo. Hivyo EWURA imevifungia vituo vya Camel Oil kilichopo Msamvu mkoani Morogoro na Matemba kilichopo Turiani kwa kipindi cha miezi sita.

Aidha ameeleza kuwa EWURA inaendelea kufanyia uchunguzi kwa vituo 10 juu ya utetezi utakaowasilishwa na vikibainika kukiuka masharti ya leseni vitachukuliwa hatua kali ikiwemo kufungiwa miezi sita.

 

No comments