Breaking News

TMA YAONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA MKUTANO MKUU WA KUMI NA TISA WA SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI

Geneva, Uswiss
KUswissaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Ladislaus Chang’a, ameongoza Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano Mkuu wa kumi na tisa wa WMO uliofanyika Geneva, Uswiss kuanzia tarehe 22 Mei hadi 2 Juni, 2023.

Sambamba na masuala mengine, mkutano huo ulipitisha vipaumbele vikuu vitatu vya kimkakati vya masuala ya hali ya hewa katika kipindi cha mwaka 2024 hadi 2027. Miongoni mwa vipaumbele hivyo, kipaumbele kikuu ni utekelezaji wa programu ya Umoja wa Mataifa ya “Taarifa za tahadhari za mapema kwa wote (Early Warning for All - EW4All)”, ambayo lengo lake ni kupunguza majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa kwa kuwezesha kila mtu kupata taarifa za hali ya hewa ifikapo mwaka 2027. 

Nchi wanachama zimeaswa kuandaa mikakati ya kutekeleza EW4All na kuandaa taarifa za utekelezaji wa programu hiyo. Maeneo mengine ya kipaumbele yaliyopitishwa ni Uimarishaji wa uangazi na ubadilishanaji wa data za hali ya hewa ili kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi Sambamba na vipaumbele hivyo, mkutano wa congress wa 19 ulipitisha mpango mkakati wa WMO utakaotekelezwa katika kipindi cha 2024-2027 ambao una malengo matano (5).

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo ukiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika WMO, Dkt. Ladislaus Chang’a, ulishiriki kikamilifu na kuchangia katika masuala yaliyoafikiwa kwa manufaa ya nchi yetu na Afrika. 

Miongoni mwa masuala ambayo Tanzania ilichangia ni programu ya Kuimarisha Uangazi “Systematic Observation Financing Facility (SOFF)” inayotekelezwa katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania kwa lengo la kusaidia kuboresha uangazi ili kuwezesha upatikanaji na ubadilishanaji wa data wa hali ya hewa kwa nchi zinazoendelea. 

Akichangia kuhusiana na utekelezaji wa programu ya SOFF nchini Tanzania, Dkt. Ladislaus Chang’a alishauri WMO kuangalia upya vigezo vya jumla vilivyowekwa katika kuamua idadi ya vituo vinavyohitajika katika nchi husika vitakavyofungwa chini ya programu ya SOFF, ambapo alishauri vigezo hivyo vizingatie mazingira ya nchi husika ikiwa ni pamoja na sura ya nchi. 

Alitoa mfano wa Tanzania ambayo sura yake ya nchi ina milima na mabonde jambo linalochangia maeneo mengi kuwa na hali ya hewa inayotofautiana, hivyo maeneo hayo yanatakiwa yawe na vituo vya kufanya uangazi.

Aidha, katika mkutano wa congress wa 19 ulifanyika uchaguzi mkuu wa viongozi wa WMO katika ngazi ya Rais, Makamu wa Kwanza wa Rais, Makamu wa Pili wa Rais, Makamu wa Tatu wa Rais, Katibu Mkuu wa WMO na Wajumbe wa Baraza Kuu la Utendaji la WMO (WMO Executive Council). 

Viongozi wapya wa WMO waliochanguliwa ni Dkt. Abdulla Al Mandous (nafasi ya Rais wa WMO kutoka UAE); Dkt. Daouda Konate (nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kutoka Cote d'Ivoire); Bw.Eoin Moran (nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais kutoka Ireland); Dkt. Mrutyunjay Mohapatra (nafasi ya Makamu wa Tatu wa Rais kutoka India); na Prof. Celeste Saulo (nafasi ya Katibu Mkuu wa WMO kutoka Argentina).

Viongozi wengine waliochaguliwa ni Wajumbe 27 wa Baraza Kuu la Utendaji la WMO ambapo miongoni mwao ni Wajumbe 8 kutoka Bara la Afrika ambao ni Bw. Moegamat Ishaam Abader (Afrika ya Kusini), Dkt. David Gikungu (Kenya); Prof. Mansur Bako Matazu (Nigeria); Major General Aviator Hesham Tahoun (Misri); Bw. Simplice Tchinda Tazo (Cameroon); na Bw. Joël Zoungrana (Burkina Faso).

Kwa upande wa Viongozi wakuu waliomaliza muda wa utumishi wao ni Prof.Gerhard Adrian (aliyekuwa Rais wa WMO kutoka Ujerumani), Prof. Peteri Taalas (aliyekuwa Katibu Mkuu wa WMO kutoka Finland), Bw. Albert Martis (aliyekuwa Makamu wa Pili wa Rais kutoka Curaçao), Dkt. Agnes Kijazi (aliyekuwa Makamu wa Tatu wa Raisi kutoka Tanzania).

Katika hatua nyingine, Dkt. Chang’a alikutana na viongozi mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Taasisi za hali ya hewa za nchi wanachama wa WMO, wadau wa maendeleo (Development Partners) na viongozi wapya wa WMO ambapo alifanya nao mazungumzo kuhusiana na mashirikiano katika huduma za hali ya hewa.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa 19 wa Congress ulijumuisha washiriki 21 ambapo wanane (8) walishiriki Geneva, Uswisi na wengine 13 walishiriki kwa njia ya mtandao. 

Walioshiriki Geneva in (1) Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika WMO, Dkt. Ladislaus Chang’a, (2) Mhe. Balozi. Maimuna Tarishi, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Geneva. (3) Mhe. Balozi Hoyce Temu, Naibu Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Geneva; (4) Kaimu Mkurugenzi wa TMA Ofisi ya Zanzibar, Bw. Masoud Faki; (5) Meneja wa Mashirikiano ya Hali ya Hewa Kikanda na Kimataifa, Bw. Wilbert Muruke; (6) Mkurugenzi wa Huduma za Maji katika Wizara ya Maji, Dkt. George Lugomela (7) Mkurugenzi Msaidizi katika Wizara ya Maji, Bw. Robert Sunday; na (8) Bi. Zulekha Fundi, Afisa wa Ubalozi, Geneva

No comments