RIPOTI MAALUM: UPATU "Smart Phone" JANGA JIPYA KWA WANAFUNZI WA SEKONDARI
By George Helahela
Je, umewahi kuona wanafunzi wakiwa wamerundikana katika kituo cha daladala huku wakiyaacha mabasi ya abiria hata kama ni matupu? Unajua siri iliyojificha miongoni mwao kama sio wengi wao? Mwananchi Digital imefanya uchunguzi wa kina na kubaini chanzo.
Uchunguzi wa takribani mwezi mzima umebaini kuwa idadi kubwa ya wanafunzi wa jijini hapa hususani wasichana wanajihusisha na michezo ya upatu shuleni kiasi cha kutumia fedha za kujikimu na hata nauli hivyo kukabiliwa na changamoto ya kushinda njaa na kukosa nauli na matokeo yake ni wengi wao kupoteza muda mwingi vituoni wakiomba lifti kwenye magari binafsi, malori ya mchanga na magari madogo ya mizigo ‘Kirikuu’.
Hamida Ngombile (si jina halisi) mwanafunzi kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Kwembe anasema hulazimika kuomba lifti kwa kuwa fedha anazopewa nyumbani huishia kwenye upatu. “Fedha ninayopewa hainitoshi. Nina michezo miwili ya Sh500 kila siku, unafikiri nitapata nauli?”
Kama wahenga wasemavyo, hakuna cha bure. Lifti anazoomba Hamida zimekuwa zikimwingiza katika vishawishi kama anavyoeleza.
“Kuna wakati nikipanda lifti natongozwa au naombwa namba ya simu, nikiwapa namba wakinitafuta nawa-block.”
Tofauti na zamani ambako walikuwa huru kushiriki mchezo huo shuleni, Hamida anasema kwa sasa ni ngumu kwa sababu walimu wanawatumia wanafunzi wengine kuchunguza hivyo wameuhamishia mtaani kauli ambayo inashabihiana na ile ya Mkuu wa Shule ya Sekondari Kwembe, Aloyce Buloto ambaye anasema michezo ya upatu na kamari kwa wanafunzi wake imepungua kwa kiwango kikubwa kutokana na adhabu zilizopangwa.
“Tumeweka sheria kwa wanafunzi kutojihusisha na michezo yoyote ya kamari na upatu. Endapo akikamatwa atapewa adhabu kali ikiwamo kurudishwa nyumbani na tunashirikiana na askari wa mtaa katika kutekeleza hilo,” anasema na kuongeza; “wanafunzi wakikamatwa huko mtaani na askari kata, wazazi wao watalazimika kulipa faini. Kimsingi tabia hizi zimepungua sana, hata walimu wanajitahidi kufuatilia matukio kama haya ili yasiwepo shuleni.”
Kama ulidhani hili ni tatizo la Wilaya ya Ubungo ilipo Sekondari ya Kwembe pekee utakuwa umekosea. Mwananchi Digital pia ilifanya mahojiano na Josephine Pukwa (naye sio jina lake halisi) mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mchikichini, Wilaya ya Ilala ambaye anasema naye ni miongoni mwa wanaocheza upatu lakini kwa tahadhari kubwa.
“Shuleni hawaruhusu na endapo mtabainika mnarudishwa nyumbani kwa wiki tatu. Hata kidato cha nne waliomaliza waliwahi kukamatwa kwa hiyo tunafanya kwa siri sana.”
Josephine ambaye sasa yupo kidato cha nne anasema fedha za upatu anazipata kwa wazazi ikiwa ni nauli na fedha za chakula anazopewa kila siku.
Usiri anaouzungumzia Josephine unathibitishwa na Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mchikichini, Julieth Masalu ambaye anasema wameudhibiti vilivyo katika mazingira ya shule.
“Kwa sasa hawazifanyi hizo tabia hapa shuleni labda nyumbani, kwa sababu mwaka jana tulikuwa na kesi kama hiyo ya wanafunzi kucheza upatu na ilijulikana baada ya kijumbe (mtunza fedha za upatu) kula fedha za wenzake na tuliwapa adhabu,” anasema Mwalimu Julieth. Anasema wanafunzi hao walipokamatwa walisimamishwa masomo.
Kijumbe
Habari za kuwapo kwa kijumbe ziliifanya Mwananchi Digital kumtafuta mmoja wao na kumpata mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Sekondari Mchikichini aliyejitambulisha kwa jina moja la Shamim (18) ambaye anasema amekuwa akifanya shughuli hiyo tangu akiwa kidato cha kwanza. Pamoja na udhibiti uliowekwa shuleni hapo, binti huyo anasema anaendesha michezo miwili ya upatu hapo Sekondari ya Mchikichini.
“Ninachezesha michezo miwili; kuna wa Sh300 kila siku na Sh500 kila siku, kwa wiki wanatoka (wanapewa fedha) watu wawili,”anasema.
Hivi anafafanua kuwa kwa wiki mshiriki mmoja hupata Sh70,000 hadi Sh80,000 kutegemea na mchango aliomo, “Darasani wasichana wanaocheza wapo 110 kwa mikondo yote na kuna ambao wanacheza kwa majina hadi matatu,” anaongeza.
Kama umezoea michezo ya upatu ya mtaani kuwa fedha zinatunzwa kwenye simu au benki basi hapa ni tofauti, Shamim anasema fedha huzitunza katika mkebe wake ambao muda wote anatembea nao ndani ya begi lake la madaftari.
“Nina mkebe wangu natembea nao kila sehemu na nauweka kwenye begi la shule na naliweka mbele, fedha zote zinakuwa humo,” anasimulia.
Kutokana na majumu hayo ya ziada aliyojipa, Shamim anasema inamlazimu kuchelewa kurudi nyumbani kila siku akifuatilia fedha za mchezo kwa wanafunzi wa mikondo mingine ambao ratiba zao za masomo ni tofauti ili akabidhi kwa mhusika anayepokea wiki hiyo.
Ni fedha wanazopewa nyumbani tu?
Uchunguzi wa Mwananchi Digital umebaini kuwa ingawa wapo wanaojibana na kutumia fedha wanazopewa kwa nauli na chakula kama ilivyo kwa Hamida na Josephine idadi kubwa wanapata fedha hizo kutoka kwa watu wanaohusiana nao kimapenzi na hilo linapigiliwa msumari na Shamim.
“Kila mtu anayecheza ana sehemu yake ya kupata fedha, ila wengi wanabana fedha zao za matumizi na wengine wanapata kwa wachumba zao ambao wengine wanasoma nao darasani au watu wa mtaani kama bodaboda,” anasema.
Shamim anasema wanafunzi wengi akiwamo wanapopata fedha hizo hupenda kununua simu janja (smartphone) na sare za madera kwa ajili ya shughuli za mtaani ikiwamo sherehe za siku ya kuzaliwa, kitchen part na harusi… “hayo ndio mambo yetu uswazi,” anasema.
Wazazi wanajua?
Shamim anayeishi Mwananyamala Kwa Mama Zakaria anasema awali mzazi wake alikuwa hajui kama anacheza upatu lakini siku moja alikwama na akamkopesha ambako alimweleza chanzo cha fedha hizo baada ya hapo hakuwa na shida.
“Nilimuazima Sh40, 000. Unajua mama yangu tangu nasoma shule ya msingi alikuwa kijumbe mtaani kwetu kwa hiyo hasumbui (hana shida),” anasema kwa kujiamini.
Kauli ya Shamin inaungwa mkono na Mwalimu Julieth ambaye anasema mtindo wa maisha wa sehemu ambazo wanafunzi wake wengi wa wanaishi na wazazi wao ndicho chanzo.
“Karibu asilimia 70 ya wanafunzi wanaosoma hapa wanatokea Buguruni na Vingunguti sehemu ambazo mtindo wa maisha wake unawaathiri, wanaiga kucheza upatu kutoka kwa wazazi wao kwa sababu wamekuwa wakiwaona tangu utotoni,” anasema.
Wizara yashtuka
Licha ya mchezo huo kuonekana kuota mizizi katika shule nyingi za Dar es Salam, Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mtahabwa anasema hawajawahi kusikia wala kuona ripoti ya jambo hilo.
“Suala hili ndio kwanza nalisikia kwako kwa mara ya kwanza. Tafadhali kama una majina ya hizo shule nipatie nilifanyie kazi,” akiongeza kwamba tabia za aina hiyo (za michezo ya upatu shuleni) zina mwelekeo hatarishi kwa wanafunzi.
“Lengo letu kama wizara ni kuhakikisha wanafunzi wanajikita katika taaluma na si vinginevyo. Hapo kwenye matumizi ya simu ni hatarishi sana kwa wanafunzi, nitalifuatilia hilo ili tuweze kulikomesha mara moja.”
Mtaani hali ikoje?
Yale ambayo Mwananchi Digital iliyabaini huko Kwembe na Mchikichini si mageni pia kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Chekechea uliopo katika Kata ya Mikwambe wilayani Kigamboni ambako mwenyekiti wake, Abdallah Kindamba anasema, “wanafunzi wengi wanaoongoza kuomba lifti ni wasichana. Wanadai kuwa fedha hazitoshi lakini tumebaini huenda kuna vitu vyao vingine binafsi wanafanya katika fedha wanazopatiwa.”
Mbali ya Kindamba shuhuda mwingine ni Ramadhani Mape, mzazi na mfanyabiashara Soko la Makumbusho. Anasema amewahi kushuhudia wanafunzi wakizungumzia michezo ya upatu na kwa mtazamo wake, hiyo inawaingiza kwenye uhuni.
“Watoto wengine wanasoma mbali, mfano mimi ninatoka Vingunguti asubuhi nikiwa nakuja kwenye biashara zangu ninapanda na watoto wa shule za sekondari ambao wanasoma Ilala, sasa hapo mzazi lazima ampatie mtoto fedha ya nauli na chakula,” anasema.
“Lakini akimpa yeye anacheza upatu Sh500 kila siku, kwa hiyo unawakuta vituo vya mabasi wanaomba lifti. Michezo hii wanafanya kwa sababu gani? Mimi naona inawafanya wawe wahuni.”
Kuhusu malezi ya wazazi; Mape anasema “Sidhani kama wazazi hawawalindi, lakini mambo hayo wanayafanya sana wakiwa shule kwa sababu mambo wanayotaka makubwa. Wakicheza mchezo wanapata kijola (dera) na ananunua simu janja,” alisema.
Sophia Hamisi ambaye ni mama lishe wa Kawe Beach na mzazi wa binti anayesoma sekondari anasema wanafunzi kucheza upatu hakuleti picha nzuri na kuna athari za kitaaluma.
“Hiyo sio tabia nzuri hata kidogo na haileti picha nzuri, watoto wa sekondari sasa hivi wana tabia ambazo usipofuatilia kwa umakini kama mzazi utaletewa mjukuu mapema,” anasema.
Mgogoro kwenye daladala
Uchunguzi wa Mwananchi Digital umebaini kuwa athari za upatu zimekuwa zikiibua mgogoro baina ya wanafunzi na makondakta wa daladala. Kondakta wa daladala ya Buza- Makumbusho Ibrahim Omari anasema utoaji wa nauli wa wanafunzi hasa wasichana sio wa kuaminika kwa sababu mara kadhaa huomba kupanda bure.
“Wanafunzi wa sekondari hawaeleweki mara siku nyingine waseme wanayo siku nyingine hawana (nauli), nasikia wanacheza michezo ya kupeana fedha huko shuleni,” anasema.
Akizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, dereva wa daladala inayofanya safari zake Makumbusho kwenda Bunju anasema mzizi wa tatizo hilo ni wazazi hasa wanawake kwa sababu wanawatunzia siri watoto wao.
“Wanawafichia mambo yao hawa mabinti zetu, hilo mimi naliona. Yaani mtoto anasoma anamiliki ‘smartphone’ na mama anajua lakini hamuulizi chochote, kuharibika kwa wanafunzi kosa ni la wazazi,” anasema.
“Watoto wanaenda shule wakiwa na nguo mbilimbili, wanaingia kwenye upatu kwa sababu na yeye anataka kununua simu kubwa ya laki tatu kama mwenzangu na wakati mwingine hadi mzazi anaombwa fedha ya kwenda kulipia mchezo (upatu), malezi bado ni tatizo,” anaongeza.
Wanasaikolojia wanalizungumziaje jambo hili?
Naima Omari, mwanasaikolojia na mtoa ushauri anasema wanafunzi hao wamewaiga wazazi wao kwani wanaona wanachokifanya.
Lakini anaonya kuwa tabia hizo zinamuondoa mwanafunzi katika utulivu wa kuzingatia masomo na anaweza kufeli katika mitihani.
“Saikolojia ya mtoto inahitaji utulivu ili aweze kufanikiwa katika jambo analolifanya. Sasa kama anasoma na bado anawaza atapata wapi fedha ya kulipia upatu hii inamuweka katika mazingira ya kufeli masomo,” anasema.
Mdau wa masuala ya familia na mahusiano, Neema Lyimo anahoji miaka 20 ijayo kutakuwa na taifa la aina gani? “Unajua hili jambo linaweza kuonwa ni la kawaida, lakini piga picha ya miaka 20 ijayo, tutakuwa na taifa la namna gani? Hivi mtoto acheze upatu, mawazo yatakuwa kutafuta hela, masomo yatawekwa pembeni na ni wazi watajiingiza kwenye mahusiano ili wapate pesa za michezo hiyo.”
Neema anaamini kwamba ni wakati sasa kwa wazazi, walimu na wadau wote wa elimu ikiwamo Serikali, kutafuta namna bora ya kuondokana na tatizo hili. “Ingekuwa ni amri yangu, watoto wote wa kike wangesoma bweni, labda ingepunguza mambo haya.”
Source Mwananchi
No comments