Breaking News

BRELA YAHIMIZWA KUSAIDIA WANANCHI

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imehimizwa kuwasaidia wananchi waliopo mkoa wa Tanga ili waweze kurasimisha biashara zao. 

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Uwezeshaji na Maendeleo ya Sekta Binafsi, Bw. Conrad Millinga kutoka Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, ambaye amemwakilisha Waziri  wa Wizara hiyo Mhe. Ashatu Kijaji,   alipotembelea banda la BRELA kwenye Maonesho ya 10 ya Biashara na Utalii yanayofanyika katika Uwanja wa Mwahako jijini Tanga. 

Bw. Millinga amesisitiza kuwa ushiriki wa BRELA kwenye Maonesho hayo utoe matokeo chanya kwa kutoa usaidizi wa karibu kwa wananchi ili waweze  kurasimishwa na kupata huduma zingine. 

"BRELA ni lango la biashara,  ambapo mfanyabiashara yeyote awe na mtaji mkubwa au mdogo ni muhimu kurasimisha biashara, hivyo wafanyabiashara wapatiwe usaidizi wa karibu kwenye mfumo wa Usajili ambao unafanyika  kwa njia ya Mtandao, ili baadaye waweze kuchangia pato la taifa" amesisitiza Bw. Millinga.

Naye Afisa Leseni wa BRELA, Bw. Jubilate Muro,  amemhakikishia kuwa ushiriki wa BRELA utaleta matokeo chanya kwakuwa imedhamiria kutoa usaidizi wa karibu kwa wafanyabiashara na zaidi kutoa elimu kwa wadau wanaotembelea banda la BRELA pamoja na kushiriki katika vipindi  vinavyorushwa kupitia  radio na televisheni za jijini humo.
 
Katika maonesho hayo BRELA  inatoa huduma mbalimbali za Sajili, utoaji wa Leseni na huduma baada ya Sajili. Maonesho haya yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 6 Juni, 2023.

No comments