Breaking News

TMA YATOA UTABIRI WA MSIMU WA KIPUPWE, MAENEO MENGI YA NCHI KUWA NA JOTO KIASI HADI BARIDI YA WASTANI

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema katika kipindi cha Juni hadi Agosti (JJA) 2023 hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi.

Akizingumza leo Mei 26, 2023 na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Ladislaus Chang’a wakati akitoa taarifa kuhusu Mwelekeo wa Hali ya Hewa kwa Kipindi cha Juni Hadi Agosti Mwaka huu.

“Hata hivyo, hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo ya Nyanda za Juu Kusini -Magharibi pamoja na ukanda wa Ziwa Victoria. Aidha, vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa kujitokeza mwezi Juni,” amesema Dkt. Chang’a.

Kuhusu Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Shinyanga na Simiyu) Dkt. Chang’a ameeleza kwamba hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi.

Kwamba kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 13 oC na 19 oC.

Kwa Ukanda wa Pwani ya Kaskazini (Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, maeneo ya kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba) Dkt. Chang'a amebainisha kuwa hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi.

Kwamba kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 22oC na 26oC kwa maeneo ya mwambao wa Pwani na visiwani na kati ya nyuzi joto 19oC na 22oC katika maeneo ya nchi kavu.

Hata hivyo, amesema maeneno yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 19oC.

Amesema kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara) hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi, kiwango hicho kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 13 oC na 21 oC na maeneno yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 13 oC.

Kanda ya Magharibi (Mikoa ya Tabora, Rukwa, Katavi na Kigoma) Dkt. Chang’a ameeleza hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 15 oC na 19 oC.

Kanda ya kati (Mikoa ya Singida na Dodoma) hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 14oC na 19oC.

Kwa upemde wa Ukanda wa pwani ya kusini  (Mikoa ya Mtwara na Lindi) amesema hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 16 oC na 22 oC.

Na Kanda ya kusini (Mkoa wa Ruvuma) akieleza kuwa hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto linatarajiwa kuwa  kati ya nyuzi joto 11oC na 16 oC.

Kanda ya Nyanda za juu Kusini - Magharibi (Mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe pamoja na maeneo ya kusini ya Mkoa wa Morogoro amesema hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 7 oC na 16 oC wakati katika maeneo ya miinuko kiwango hicho kinatarajiwa kuwa chini ya nyuzi joto 7 oC.
Akizungumzia kuhusu mwenendo wa upepo kwa kipindi cha Juni hadi Agosti Mwaka huu Dkt. Chang’a amesma kwa kawaida msimu wa Kipupwe hutawaliwa na upepo wa Kusi.

Alisema msimu wa huu unatarajiwa kuwa na upepo utakaovuma kutoka Kusini-mashariki na Mashariki (Matlai) katika Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu.

“Kwa ujumla, upepo wa wastani unatarajiwa kushamiri katika maeneo mengi nchini,” ameeleza Dkt. Chang’a.

Kuhusu mwelekeo wa mvua kwa kipindi cha Juni hadi Agosti Dkt. Chang’a amesema kwa kawaida kipindi cha JJA kinatawaliwa na hali ya ukavu katika maeneo mengi ya nchi.

Hata hivyo, ameeleza upepo kutoka Kusini-Mashariki hadi Mashariki unatarajiwa kuleta unyevunyevu kutoka katika Bahari ya Hindi ambao unaweza kusababisha vipindi vya mvua katika maeneo machache ya ukanda wa pwani (mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, Morogoro, Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba).

No comments