Breaking News

TAKUKURU TEMEKE YAMPA TANO MKURUGENZI TEMEKE KUSITISHA MAKATO YA WAALIMU KWENDA CWT

Dar es Salaam:
Wanachama wa Chama cha Kuwalinda na Kutetea Haki za Walimu Manispaa ya Temeke wametoa pongezi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya hiyo bwana Elihuruma Mabelya kufatia kutekeleza ushauri wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Temeke wa kusitisha makato ya kuchangia Vyama viwili vya walimu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Temeke bwana Holle Makungu amesema uamuzi huo umefikiwa kufatia kuwepo na vyama viwili vya walimu ambavyo amevitaja kuwa ni Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na Chama cha Kuwalinda na Kutetea Haki za Walimu (CHAKUHAWATA).

Alisema awali Walimu waliwasilisha malalamiko yao Takukuru kuwa wamekuwa wakikatwa mishahara yao na kuchangia Vyama viwili kinyume na kifungu cha 61 (1) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini namba 6 ya Mwaka 2004 ambayo inampa uhuru mfanyakazi kuchagua makato yake yaelekezwe kwenye Chama gani cha wafanyakazi anachoona kinamfaa.

“Kwa mujibu wa Kifungu hicho cha Sheria kikisomeka pamoja na Kanuni ya 37 ya Kanuni za Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya Mwaka 2007 havikutafasiriwa vizuri na watendaji wa Manispaa ya Temeke kiasi kwamba Walimu hao waliendelea kukatwa asilimia 2 ya mishahara yao na kupelekwa CWT wakati walishajiondoa kwenye chama hicho na walistahili kukatwa kupitia CHAKUWAHATA pekee,” Alisema Bw. Makungu

Bw alibainisha kuwa Kupitia kazi za uzuiaji Rushwa kwa maana ya dhana ya Takukuru rafiki na kwa kuzingatia kifungu cha 7 Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na 11/2007 tulimshauri Mkurugenzi kuhusu kadhia hiyo ambayo imekuwa ikiwapata Walimu hao na baada ya kupata ushauri huo alisitisha mara moja Makato hayo.

Akizungumzia kuhusu ufatiliaji juu ya Rushwa amesema ufuatiliaji wa Miradi na Matumizi ya mikopo ya asilimia 10 ya Mapato ya Halmashauri wamebaini kuwepo dosari mbalimbali katika pande zote mbili za wakopaji na wakopeshaji (Manispaa ya Temeke).

Ametaja dosari hizo kuwa ni pamoja na baadhi ya vikundi kupewa mikopo isiyo kidhi malengo ya wanakikundi ambayo yaliwekwa kwenye andiko la mradi wao.

“Mfano kikundi kinaomba mkopo mkubwa (sh. 60,000,000/=) wakiwa na matarajio ya kufungua Mradi mkubwa kama vile duka kubwa mathalani duka la kuuza vifaa Tiba kulifungua sehemu Lakini walipewa Milioni 27 tu ambazo hazikukidhi mahitaji na malengo ya wanakikundi na biashara yao,” Alisema Bw Makungu.

Ametaja Dosari nyingine kuwa ni baadhi ya vikundi kubadilisha biashara baada ya kupata mkopo, kwa mathalani Milioni 21 kwa ajili ya kuuza na kusaga nafaka, lakini baada ya kupata mkopo hawanunui mashine ya kusaga nafaka na badala yake wananunua nafaka na kwenda kuzisagisha kwa wafanyabiashara wengine wenye mashine hizo.

Amesema takukuru mkoa wa temeke pia walifatilia utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo 10 yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 14 katika ufuatiliaji huo Miradi Sita (6) yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 9 ilibainika kuwa na mapungufu.

No comments