MBIBO AWASHAURI WACHIMBAJI WADOGO KUVITUMIA VITUO VYA MFANO
Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Dhahabu wameshauriwa kuvitumia Vituo vya Mfano vilivyojengwa na Serikali katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuwawezesha kujifunza namna bora ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini hayo ili kuongeza tija na ufanisi katika shughuli zao.
Hayo yamebainishwa leo Mei 17, 2923 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo baada ya kutembelea Vituo vya Mfano vya Lwamgasa na Katente vilivyopo Mkoani Geita.
Mbibo amesema Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kuwalea Wachimbaji Wadogo ili wafuzu kutoka kwenye uchimbaji mdogo kwenda wa kati na hatimaye kwenda kwenye uchimbaji mkubwa.
Aidha, Mbibo ametumia fursa hiyo kuzungumza na watumishi wa vituo hivyo ambapo watumishi wamemwelezewa changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi hao ikiwa ni pamoja na uhitaji wa upanuzi wa vituo hivyo ambavyo kwa sasa vina wateja wengi wanaohitaji huduma kutoka katika vituo hivyo.
Kwa upande wake, Meneja na Msimamizi Mkuu wa Vituo vya Mfano wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Tuna Bandoma amesema tangu kuanzishwa kwa kituo cha Lwamgasa takribani wachimbaji wadogo 1,948 wamepata mafunzo ya vitendo.
Aidha, Bandoma amesema jumla ya mbale tani 2,970 zimechakatwa katika mtambo wa kituo hicho ambapo jumla ya gramu 36, 791.36 za dhahabu zilizalishwa katika kituo hicho zenye thamani ya shilingi bilioni 4.322.
Awali, Mbibo alitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita na kukutana na Katibu Tawala wa Mkoa huo Prof. Godius Kanyarara akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali, Mhandisi Uchenjuaji Ruben Mdoe, Meneja wa Vituo vya Mfano Tuna Bandoma na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita Martin Shija.
No comments