Breaking News

FILAMU ZA HOLLYWOOD KUTUMIA "LOCATION" ZA UTALII TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Los Angeles, California
Maeneo mbalimbali ya kuvutia nchini Tanzania huenda yakapata fursa ya kuonekana katika filamu mbalimbali kubwa za Hollywood ili kuutangaza zaidi utalii wa Tanzania.

Akizungumza na Katibu Mkuu-Utalii aliyetembelea studio mashuhuri duniani za kuzalisha filamu jiji Loss Angeles za Paramount Studios, Makamu wa Rais wa kampuni ya Paramount Pictures, inayomiliki studio hizo, anayeshughulikia Mipango na Uhusiano na Serikali, Sharon Keyser, amesema Tanzania ni nchi nzuri ambayo kampuni hiyo ingependa kufungua majadiliano ili kuitumia katika filamu mbalimbali.

Paramount ni kampuni kubwa ya kwanza kuanzisha studio ya kuandaa filamu Hollywood mwaka 1912 na mpaka sasa imezalisha na/au kusambaza baadhi ya filamu kubwa duniani ikiwemo Titanic, The Godfather, Forest Gump, Apocalypse, Gladiator na nyingine mamia kwa mamia. 

“Tutaendelea na mazungumzo nanyi katika siku zijazo ili kulielewa zaidi soko na mfumo wenu wa nafuu za kikodi kwa sekta ya filamu ili tuweze kunufaika na mandhari nzuri mlizonazo,” alisema Bi. Sharon.
Pamoja na filamu ya “Tanzania; The Royal Tour” filamu chache sana zimeshatumia mandhari ya Tanzania ikiwemo: Tanzania: A Journey Within (2011) na The Honeymoon (2023).

Ujio wa kampuni kubwa kama Paramount unaweza kuitangaza zaidi Tanzania kiutalii kimataifa kwa kasi zaidi na kukuza pia kiwanda cha filamu nchini.

Katika hatua nyingine Dkt. Abbasi amekutana na kufanya mazungumzo ya namna ya kuutangaza zaidi utalii wa Tanzania kwa njia ya picha za kisasa na kitaalamu na mpigapicha mashuhuri wa Hollywood, Bi Karen Ballard.

Karen pamoja na kuwa mpigapicha rasmi wa filamu za Royal Tour za Rwanda (2018), Poland (2019) na Tanzania (2022) pia hufanyakazi na mastaa wakubwa wa filamu wa hapa ikiwemo kushiriki akiwa mpigapicha rasmi katika filamu ya “The Expendables” yenye mastaa kama Rambo, Jet Li, Dolph Lundgren, Bruce Willis, Arnold Schwarzenegger, Jean-Claude Van Damme na Harrison Ford. 

Bi. Karen pia hufanyakazi na makampuni makubwa ya Hollywood ikiwemo Warner Bros, Paramount, Universal, Sony, Netflix, Amazon na Apple na kabla ya hapo amefanyakazi akiripoti matukio ya Ikulu ya Marekani kwa zaidi ya miaka 10 ikiwemo picha zake kutumika rasmi katika kitabu cha “Barack Obama: The Official Inaugural Book.”

Maelezo ya picha: Fungua (swipe) kulia ni matukio ya picha mbalimbali za  kihistoria za Bi. Karen katika matukio mbalimbali makubwa duniani.

No comments