Breaking News

ACT WAZALENDO WAITAKA SERIKALI KUSIMAMIA UWEKEZAJI NA UJENZI WA VIWANDA UNAOTEGEMEA MALIGHAFI ZA NDANI

Waziri Kivuli wa Madini Mhandisi Francis Mkosamali akifafanua jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hoja saba za hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 kwa niaba ya Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara wa chama hicho jijini Dar es Salaam.

Dar es salaam:
CHAMA ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kuhakikisha inasimamia uwekezaji na ujenzi wa viwanda unaotegemea zaidi malighafi kutoka ndani.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 5, 2023 na Waziri Kivuli wa Madini wa ACT Wazalendo Mhandisi Francis Mkosamali akiwasilisha hoja saba kuhusu hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 kwa niaba ya Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara wa chama hicho.

Mhandisi Mkosamali amesema msingi wa hoja hiyo ni Sekta ya Viwanda kutofungamana vya kutosha na uzalishaji wa malighafi za kilimo, uvuvi na Madini.

Hivyo ametumia fursa hiyo kuitaka pia, Serikali kufungamanisha uendelezaji wa viwanda na sekta ya madini hususani makaa ya mawe na chuma kwa kuharakisha utekelezaji wa Mradi Linganga na Mchuchuma.

Mhandisi Mkosamali amesema katika historia ya nchi yetu na nchi nyingine nyingi Afrika hususani katika dunia ya tatu ajenda ya viwanda kwa muda mrefu imekuwa ikijadiliwa kwa namna tofauti tofauti.

“Katika kufuatilia hotuba ya bajeti na mipango ya wizara kwa mwaka huu, ina ukosefu wa mahusiano na uwiano mdogo sana wa malengo ya ujenzi/ uwekezaji wa viwanda na sekta ya uzalishaji wa malighafi hususani kilimo,” amesema Mhandisi Mkosamali na kuongeza,

“Hakuna viwanda vya kutosha kujikita katika usindikaji wa mazao ya kilimo (hususani mazao mkakati) na uzalishaji wa bidhaa muhimu kwa kutumia malighafi zinazopatikana nchini. Shabaha ya sasa ya uwekezaji na uendelezaji wa viwanda sio katika kujenga uwezo wetu wa nchi kujinasua katika hali ya utegemezi,”.

Kwamba Takwimu za viwanda kwa mujibu wa wizara ni kuwa tuna viwanda vidogo sana 62,400 sawa na asilimia 77.07, viwanda vidogo ni 17,274 navyo vinachukua asilimia 21.33 na viwanda vya kati vipo 684 sawa na asilimia 0.84 na viwanda vikubwa vipo 618 sawa na asilimia 0.76.

Kwamba licha ya takwimu hizi bado mazao mengi yanapotea shambani haizidi hata asilimia 20 ya viwanda hivyo vyenye mafungamano ya moja kwa moja na kilimo, uhakika wa masoko ya wakulima wetu bado ni mdogo sana. Mazao kama ya kahawa, pamba, chai, ufuta, korosho na chikichi ndio mazao yanayoongozwa kuuzwa nje na kwenda kuwa malighafi katika viwanda vya nchi zingine huku nchi yetu ikibaki na uhitaji wa Bidhaa zinazotokana na mazao hayo, wakulima wa mazao mengine kama machungwa, nanasi, embe, tikiti na parachichi nao hawaoni mwanga wowote wa kuwakwamua kutupa Mazao yao kila msimu kwa kukosa soko.

Amesema kwa upande mwingine, hakuna viwanda vya kutosha vya kuzalisha bidhaa za kutosha kuhudumia Sekta ya kilimo, bado mbolea kwa sehemu kubwa inaagizwa kutoka nje hadi Februari, 2023 mahitaji ya mbolea ilikuwa ni tani 698,260.

“Huku uzalishaji wa ndani ni tani 28,672 sawa na asilimia 4.1. Aidha, viuatilifu na viuwadudu (petsides and insectside) kwa sehemu kubwa vinaingizwa kutoka nje. Aidha, vifaa na zana za kilimo kwa sehemu kubwa zinatoka nje, viwanda vyetu havijibu mahitaji na soko la kilimo. Kwa maneno mengine, Sekta ya Viwanda na Sekta za Kilimo na Uvuvi zinatembea njia tofauti, jambo hili halina Afya katika maendeleo ya Taifa,”.

Kwamba Waziri Dkt. Ashatu Kijaji hakuliambia Bunge mkakati wao kama Wizara wa Kuhakikisha Zana za Kilimo na Pembejeo nyengine zaidi ya Mbolea zinazalishwa nchini, hiyo inamaanisha kuwa Wakulima wataendelea kuumia kwa kuzalisha kwa gharama kubwa zaidi zinazotokana na Pembejeo na kidogo watakachovuna hawatakua na Uhakika wa Viwanda vya kununua hapa nchini.

Amesema katika bajeti ya Serikali mwaka huu, fedha zilizotengwa kuendeleza viwanda vinavyoweza kuleta uhusiano na uwiano na sekta za uzalishaji bado ni kidogo, hivyo haiwezi kukidhi shabaha ya kufungamanisha uzalishaji na maendeleo ya viwanda.

“Kilimo na viwanda ni pande mbili za sarafu moja, ni lazima vifungamanishwe. Katika Ilani ya ACT Wazalendo 2020 tulisema “Tutafungamanisha sekta ya kilimo na sekta ya viwanda, kwa kuhakikisha kwamba viwanda vya ndani vinapata zaidi ya asilimia 80 ya mahitaji yao kutoka kwa wakulima, na kwamba wakulima wanafaidi bei nzuri ya mazao yao na soko la uhakika,”,”.

Maeneo mengine yaliyoangaziwa kwa uchambuzi ni Mchango mdogo wa Sekta ya viwanda katika pato la taifa na ajira, Mazingira ya biashara kwa Wafanyabiashara wadogo (Machinga) sio mazuri, Kufufua viwanda vya kuzalisha bidhaa zinazoweza kukidhi mahitaji ya ndani, Kupanda kwa bei za bidhaa muhimu nchini, Mfumo mbovu wa Stakabadhi za Ghalani na Mgogoro wa utwaaji wa Kiwanda cha Saruji cha Tanga 

No comments