Breaking News

SERIKALI YAENDELEA KUSISITIZA KAMPUNI ZA UCHIMBAJI WA MADINI KUSHIRIKI KATIKA SHUGHULI ZA KIJAMII

Serikali imezielekeza kampuni za uchimbaji wa madini kuhakikisha zinaendelea kushiriki  katika shughuli za kijamii ili kujenga mahusiano mazuri na wananchi wanaozunguka maeneo ya migodi.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tabora,  Mhandisi Abel Madaha  wakati akielezea kuhusu fursa mbalimbali zitokanazo na Sekta ya Madini katika mkoa huo.

Amesema kuwa Tume ya Madini imepewa jukumu la kusimamia  Sheria ya Madini katika kifungu cha 22 kwa lengo la  kuhakikisha Sekta hiyo inatoa mchango wake katika Pato la Taifa sambamba na kuhakikisha wananchi wananufaika kupitia uboreshaji wa huduma za jamii unaofanywa na migodi ya madini na kushirikishwa kwenye utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini.

“Tunatoa wito kwa kampuni zote za  uchimbaji wa madini kuhakikisha  zinashiriki katika shughuli za kijamii kwa kurudisha faida ya mapato wanayopata ili kujenga mahusiano mazuri na wananchi  wanaozunguka migodi,” amesema Mhandisi Madaha

Katika hatua nyingine, Mhandisi Madaha amesisitiza kampuni za uchimbaji wa madini kuhakikisha zinatoa kipaumbele cha ajira kwa watanzania wazawa ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.


Kwa upande wake Mratibu wa Miradi wa Kampuni ya Uchimbaji Madini ya TAUR Tanzania Limited, Edith Moses amesema kuwa katika kuhakikisha wanatekeleza Sheria ya Madini tayari  kampuni imejenga madarasa mawili na vyoo katika shule ya Msingi na Sekondari Nanga iliyopo Wilaya ya Igunga mkoani Tabora.

Naye Mwendesha Mitambo wa Kampuni ya TAUR Tanzania ameongeza kuwa uwepo wa machimbo umesaidia kutoa ajira kwa vijana wengi ambapo sasa wanapata fedha ambazo zinawasaidia kuhudumia familia zao.






No comments