Breaking News

DKT MWAKYEMBE: AWATAKA VIJANA KULINDA NA KUTHAMINI MUUNGANO PAMOJA NA KULINDA MAADILI YA KITANZANIA

Waziri wa zamani na mwanasiasa Harrison Mwakyembe, amewataka vijana kulinda na kuthamini Muungano, huku akiwasisitiza kuishi na kusimamia maadili ya Kitanzania ikiwa ni kuenzi maono ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, kwasababu bila kufanya hivyo kutasababisha kuwe na taifa mfu.

Mwakyembe ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam katika Mdahalo  wa Kitaaluma  wa Chuo Cha Ustawi wa Jamii (ISW), uliyobebwa na mada isemayo ‘Maadili ya Vijana kwa Jamii’ ikiwa ni maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano.

“Tujivunie Muungano wetu na sio kwa bahati nasibu tuwe kifua mbele, tujivunie na kuulinda Muungano ndio  maana mwalimu alisema hata bila mapinduzi Tanganyika na Zanzibar ingeungana,nchi kubwa zilikiwa haziamini kama Muungano huu utadumu". 

Naye  Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho Sophia Simba, amesema wanafunzi wa chuo hicho na maofisa ustawi wa jamii nchini wanakazi kubwa ya kutengeneza mikakati na njia sahihi ya kukabiliana na mmomonyoko wa maadili.

Pia Sophia amesema jamii ifuate  misingi bora  ya malezi, na wafanye ufuatiliaji wa kutosha wa makuzi ya watoto, kwasababu itasaidia kujenga ustawi mzuri wa taifa.

Kwa upande wake  Mkuu wa chuo cha ISW Dkt. Joyce Nyoni amesema taifa likiwa na maadili mema litazidi  kudumisha hata Muungano uliyopo.

Amesema mdahalo uliyofanyika chuoni hapo umelenga kuikumbusha jamii kuhusu masuala ya maadili, kwani ni jambo la muhimu katika kuhakikisha taifa linakuwa na ustawi bora.
 

No comments