Breaking News

CUF YAUNGA MKONO MAAGIZO YA RAIS KWA KATIBU MKUU KIONGOZI KUHUSU RIPOTI YA CAG

THE CIVIC UNITED FRONT (CUF- Chama Cha Wananchi)

MAAGIZO YA RAIS KWA KATIBU MKUU KIONGOZI KUHUSU RIPOTI YA CAG:

CUF-Chama Cha Wananchi kinaafiki msimamo wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kushughulikia Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika kutibu dosari na mapungufu yaliyobainishwa.

Kauli aliyoitoa Mheshimiwa Rais ya kumtaka Katibu Mkuu Kiongozi kuwaagiza Makatibu Wakuu wa Wizara kupitia mapungufu yaliyopo kwenye Ripoti na kuyaandalia majibu ni hatua muhimu katika kuelekea kuboresha Utendaji kwa watumishi wa Umma. Hata hivyo, CUF- Chama Cha Wananchi tunapenda kukumbusha yafuatayo:-

Mapungufu yaliyomo kwenye Ripoti ya CAG yanatokana na sababu kuu tatu:-

Kwanza ni Maamuzi mabaya ya Serikali Kuu katika kutekeleza miradi kadhaa. Maamuzi ya kutumia FORCE ACCOUNT kwenye miradi kadhaa hususan ya Ujenzi ni Maamuzi mabaya kwa kuwa yanakiuka Misingi ya Ushindani katika Zabuni (Competitive Tendering) na kuchochea Ufisadi na kutowajibika. Tutarajie katika Ripoti zijazo taarifa ya kuharibika kabla ya muda wake kwa miundombinu kadhaa inayojengwa kwa utaribu huu, kwa kukosa ubora. Tiba ya hili ni kurudi kwenye Utaratibu wa kuheshimu Sheria ya Manunuzi na Kanuni zake (Procurement ACT and Procurement Regulations).

Pili; kuna mapungufu ya watumishi wa Umma katika kutekeleza wajibu wao, inaweza kuwa ni kwa nia ovu ya Ufisadi au kwa uzembe tu. Kwa hili ni vema uchunguzi wa kina ukafanywa kama alivyoagiza Rais Samia ili hatimaye hatua za Kisheria na za kinidhamu pia zichukuliwe. Hata hivyo ni muhimu kuwa makini katika hili kwani uzoefu unaonesha kuna watumishi ambao hutolewa kafara kwa kufunguliwa mashitaka na kuwaacha wahusika halisi na baada ya muda mrefu wa kesi mahakamani, kesi hizo hufutwa na wale wahusika halisi wakibaki bila kuguswa.

Tatu; ni makosa yatokanayo na kukosekana kwa Utaalam Muafaka katika kuandaa, kutunza na hatimaye kuwasilisha taarifa muhimu kwa Wakaguzi wakati wa Ukaguzi. Zipo taasisi na mashirika mbalimbali ambayo Ripoti za CAG zinadhihirisha mapungufu yanayoweza kuaminika kwamba ni ubadhirifu na Ufisadi lakini ukweli ni kwamba taarifa hizo zina mapungufu kwenye Maandalizi ndani ya taasisi husika. Tiba ya hili ni kuhakikisha Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani (Internal Audit Section) inakuwepo na kuimarishwa kwa kila taasisi ya Umma. Mafunzo ya kujenga Uwezo (Capacity Building) ambayo kwa kiasi kikubwa yalidorora kuanzia Awamu ya tano, ni bora yakaendelezwa kwa Watendaji muhimu wanaohusika na miradi, fedha na ukaguzi.

Hata hivyo, CUF- Chama Cha Wananchi kinapongeza kazi nzuri iliyofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na pia kwa jinsi Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alivyodhihirisha kuguswa na Ripoti hii na hatua anazoonesha kukusudia kuzichukua.

HAKI SAWA NA FURAHA KWA WOTE!

Eng. Mohamed Ngulangwa
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma CUF- Chama Cha Wananchi
Aprili 10, 2023

No comments