Breaking News

WANAFUNZI CHUNYA WAPATA ELIMU YA MADINI

Wanafunzi wa Kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari Kiwanja iliyopo wilayani Chunya wamepata fursa ya kujifunza kwa vitendo jiolojia, aina za madini na aina za miamba inayopatika katika mkoa wa Kimadini Chunya.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Kamishna Msaidizi wa Uongezaji Thamani Madini kutoka Wizara ya Madini Bartha Luzabiko ametoa wito kwa shule nyingine tutembelea banda la Wizara ya Madini lililopo  katika Maonesho ya Kwanza ya Teknolojia ya Madini Mkoa wa Mbeya ili kujifunza tabia mbalimbali za madini na mnyororo mzima wa shughuli za madini.

Pia, wanafunzi hao wamejifunza kuhusiana na utunzaji wa mazingira, afya na usalama mahali pa kazi, upatikanaji wa leseni pamoja na ushiriki wa watanzania katika uchumi wa madini. 

Vilevile, wanafunzi hao wamepata nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali na kupatiwa majibu ya papo hapo ambapo Mwalimu wa Shule hiyo Adela Nhwaga ameipongeza Wizara ya Madini kwa kutoa elimu kwa wanafunzi hao.

Katika hatua nyingine,  Shule ya Msingi Kane Gold School imetembelea Banda la wizara hiyo ambapo wamepata fursa ya kutazama aina mbalimbali za madini ikiwemo dhahabu, makaa ya mawe, Kwatsi, mabo na madini ya risasi.

Maonesho ya Kwanza ya Teknolojia ya Madini Mkoa wa Mbeya yanayoendelea katika viwanja vya Sinjiriri katika Mkoa wa Kimadini Chunya yamebebwa na Kaulimbiu isemayo Uongezaji Thamani Madini kwa Maendeleo ya Taifa".








No comments