MAREKANI YAONESHA UTAYARI KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KUENDELEZA MADINI YA KIMKAKATI
Dar Es Salaam
Serikali za Tanzania na Marekani zimejadili namna zinavyoweza kushirikiana katika Uendelezaji wa Madini ya Kimkakati yanayopatikana nchini ili kuiwezesha Tanzania kuzalisha madini hayo kwa wingi.
Maeneo ya ushirikiano yaliyojadiliwa ni pamoja na kukuza uwezo wa kitaalam kwenye mnyororo wa uongezaji thamani madini ya kimkakati, kushirikiana na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) katika kuwezesha shughuli za utafiti ili kugundua mashapo zaidi ya madini hayo.
Maeneo mengine yaliyojadiliwa ni pamoja na kuongeza ushawishi kwa wawekezaji wa Marekani kuanzisha mitambo na viwanda vya kuchakata madini ndani ya nchi ili kuongeza tija kwenye uchumi, kuongeza ajira na kuwezesha Tanzania kuzalisha madini hayo kwa wingi ikiwemo bidhaa zinazotokana na madini hayo.
Akizungumza katika kikao hicho kati ya nchi hizo kilichofanyika Machi 16, 2023 jijini Dar Es Salaam, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo alisema Serikali ya Tanzania iko tayari kushirikiana na Marekani kuhakikisha taifa linanufaika na rasilimali madini ikiwemo ya kimkakati.
Naye, Afisa Ubalozi wa Serikali ya Marekani ambaye aliongoza ujumbe wa nchi hiyo Jeremy Beck, aliiomba Wizara ya Madini kuiwezesha nchi hiyo kupata taarifa zinazohusu masuala ya uwekezaji ikiwemo matakwa ya Kisheria na Mikataba inayohusu uwekezaji wa madini ya kimkakati.
Tanzania imebarikiwa kuwa na madini mengi ya kimkakati yakihusisha madini ya nikeli, kinywe, rare earth elements, colbat, chuma, bati, na mengine ambayo ndiyo yanahitajika kwa sasa duniani kwa ajili ya kutumika katika teknolojia mbalimbali ikiwemo kutengenezea simu za mkononi, kompyuta na kutengeneza mota za magari yanayotumia umeme.
Aidha, akizungumza hivi karibuni katika mdahalo wa Thamani Madini, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko alisema Serikali kupitia Wizara ya Madini tayari imeandaa mkakati na imeanza kufanya tafiti mbalimbali za madini hayo ili kujua mahali yaliko kwa kiasi gani, namna yatakavyochimbwa ikiwemo ujenzi wa viwanda vya kuyachakata hapa hapa nchini ili taifa liweze kunufaika ipasavyo.
Katika mdahalo huo, Waziri Biteko alisema si kwamba nchi imeharakishwa kuchimba madini hayo bali ni kutokana na uhitaji wa dunia.
Aidha, mwaka 2021 wakati Tanzania iliposhiriki katika Maonesho ya Expo Dubai 2020, Kamishna Jenerali wa Banda la Marekani katika maonesho hayo Robert Clark baada ya kutembelea banda la Tanzania katika maonesho hayo aliahidi kuiunganisha Tanzania na wafanyabiasha wa madini ya colbat na kueleza kuwa, Tanzania inayo fursa kubwa ya kushirikiana na nchi hiyo.
Wengine walioshiriki kikao hicho cha majadiliano ni Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam Ally Maganga, Mjiolojia kutoka ofisi hiyo Lameck Masanja na wawakilishi wengine kutoka ubalozi wa Marekani nchini.
No comments