Breaking News

WAJAWAZITO 556 KATI YA VIZAZI HAI LAKI 1 NA WATOTO WACHANGA 21 KATI YA VIZAZI HAI ELFU 1 HUPOTEZA MAISHA KILA MWAKA TANZANIA

Na. WAF - Mtwara
Takwimu za Kitaifa zinaonesha kuwa akina mama 556 hufariki kati ya vizazi hai laki moja na watoto wachanga 21 hufariki kati ya vizazi hai elfu moja  kila mwaka nchini Tanzania.

Hayo yamebainishwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Bw. Ahmed A. Ahmed wakati akifungua kikao kazi cha Kanda ya Kusini cha mwaka wa mapitio ya vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga mkoani Mtwara. 

"Kwa upande wa Kanda ya Kusini takwimu zinaonesha mwaka 2018 vifo vya akina mama vilikua 124 na mwaka 2022 kumetokea vifo 116 ambapo tumeokoa kutokea vifo 8." Amesema Bw. Ahmed 

Vilevile, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Bw. Ahmed amesema vifo hivyo vya kanda ya Kusini mwaka 2022 zinaonesha kwamba vifo 109 ambayo ni 94% kati ya vifo vyote 116 vimetokea katika vituo vya kutolea huduma baada ya akina mama kwenda kupata huduma za uzazi huku vifo 7 sawa na 6.1% vimetokea kwenye jamii kwa akina mama kujifungulia nyumbani.

Kutokana na changamoto ya kutokea kwa vifo hivyo Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendeleza mikakati ya utoaji wa elimu wa watoa huduma za Afya pamoja na jamii kwa ujumla ili kupunguza au kumaliza vifo vitokanavyo na uzazi kwa mama na mtoto.

"Kupitia kikao kazi hiki ambacho kina lengo la kufanya mapitio ya vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga niwatake mkitumie vizuri kwa kujadiliana kwa kina, kubaini sababu za vifo na muweke mpango kazi ili tuweze kubadilisha hali hii." Amesema Bw. Ahmed 

Pia, Bw. Ahmed amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imejenga Hospitali ya Kanda ya Kusini na imeanza kutoa huduma nyingi ikiwa ni pamoja na kupata madaktari bingwa ikiwemo eneo la akina mama.

Hivyo, amewataka watoa huduma kuboresha huduma za Rufaa kwa akina mama na watoto katika kanda ya Kusini kwa kuwa lengo la Wizara ya Afya ni kutoa huduma bora.

"Hatua hii itapunguza kero za kufuata huduma za kibingwa mbali kama ilivyokuwa zamani na hivyo kusaidia kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga." Amesema Bw. Ahmed 

Mwisho, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Bw. Ahmed amewataka Waganga Wakuu na watoa huduma za Afya Kanda ya Kusini kutumia majukwaa mbalimbali kwa kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kujiunga na BIMA YA AFYA KWA WOTE.

"Serikali imeanzisha mchakato huu wa Bima ya Afya kwa wote kwa kuwa ni muhimu sana hivyo, wananchi wanatakiwa kujiunga ili kufaidi matunda mazuri ya uwekezaji wa Serikali katika sekta ya Afya." Amesema Bw. Ahmed


 

No comments