Breaking News

DKT GWAJIMA: MAAFISA MAENDELEO YA JAMII ONENI NGUVU YA MICHEZO KAMA FURSA

Na WMJJWM, DSM
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima,  amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kutumia mashindano mbalimbali ya michezo kutoa elimu kwa jamii katika kubadili fikra na mitazamo ya jamii kwenye kuleta maendeleo yenye usawa wa kijinsia.

Waziri Gwajima ametoa wito  huo wakati akifungua mashindano ya riadha ya wanawake (Ladies First) Msimu wa Nne yanayofanyika viwanja vya Benjamin Mkapa, mkoani Dar es salaam Januari 21, 2023

Akizungumza na washiriki wa Mbio  hizo Dkt. Gwajima amesema anatambua kwamba wanawake bado wameachwa nyuma kwenye ushiriki wa michezo ikilinganishwa na wanaume kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo majukumu ya familia na Jamii kukosa elimu ya kutosha kuhusu ushiriki na faida za wanawake kushiriki michezo. 

"Ni dhahiri kuwa, ni vigumu kuwa na maendeleo endelevu kama wanawake ambao ni asilimia hamsini na moja (51%) ya Watanzania wote hawatashiriki ipasavyo kwenye fursa za michezo kama njia mojawapo ya kusukuma maendeleo ya kiuchumi na ajira na pia ustawi wa Afya ya jamii. Sote tutakubaliana kuwa, michezo inaleta msukumo kwenye maendeleo kwa kuwa inachangia kwenye afya bora na pia michezo ni ajira" amesema Waziri Gwajima.

Dkt. Gwajima pia, amewasihi wananchi kuona umuhimu wa kushiriki michezo mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha Afya na kujikinga na magonjwa mbalimbali ambayo ni hatarishi kwa Afya sambamba na kuonesha vipaji ambavyo vitaonekana na kuchangia katika ajira na maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla. 

"Kwa kushiriki michezo ndani na nje ya nchi ni fursa za kukutana na kufahamiana na watu mbalimbali watakaochangia maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, hivyo wanawake natoa wito tujitokeze" amesisitiza Dkt. Gwajima.  

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo Bi. Neema Msitha amesema lengo la Michezo hiyo ni kuhamasisha Wanawake kushiriki zaidi michezo.

"Chimbuko la Michezo hiyo ni uhusiano mzuri kati ya Tanzania na Japani kwenye michezo tangu mwaka 1962 na medali ya kwanza ya riadha nchini ililetwa na mwanamke"

Ufunguzi huo umehudhuriwa pia na Balozi wa Japani nchini Mhe. Ya Sushi Misawa, rais mstaafu wa chama cha riadha Juma Ikangaa, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Taifa Leodigar Tenga na Mwanariadha mstaafu Filbert Bayi ambaye aliasisi mashindano haya baada ya kupata fursa ya wadau wa Japan akijielekeza kwenye kuhakikisha yanalenga kuwainua wanawake ambapo ni mara ya nne kufanyika nchini.

Wasichana takribani 200 wanashiriki huku Kaulimbiu ya mwaka huu ni "Mwanamke Imara, Jamii Imara".







No comments