WAZIRI UMMY : UJENZI WA MADARASA WAKAMILIKA KWA ASILIMIA 95
Na: Angela Msimbira-TAMISEMI
Waziri Wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu amesema ujenzi wa madarasa 15,000 umekamilika kwa asilimia 95 katika mikoa yote ya Tanzania bara na maeneo machache hawajakamilisha kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa malighafi ya ujenzi, uchaguzi wa maeneo ya ujenzi na hali ya hewa.
Waziri Ummy amemuhakikisha Rais wa Jamhuro ya Muungano wa Tanzania kuwa hadi kufikia tarehe 15 januari, 2022 madarasa yatakuwa yamekamilika na wanafunzi wataanza masomo yao.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya UVIKO -19 Ikulu Jini Dar es salaama Waziri Ummy amesema kiasi cha shilingi bilioni 240 ziliidhinishwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 12, 000 ya shule za sekondari na bilioni 60 kwa ajili ya ujenzi madarasa ya shule shikizi za msingi na shilingi bilioni 4 kwa ajili ujenzi wa mabweni 50 kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumz
Ameendelea kufafanua kuwa kiasi cha shilingi bilioni 203.1 zilitolewa kwa ajili ya Sekta ya Afya na bilioni 5 kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kufanyia biashara kwa wafanyabiashara wadogo.
Amesema hadi kufikia tarehe 31 Disemba, 2021 kwa upande wa sekta ya elimu msingi Ofisi ya Rais TAMISEMI imepokea shilingi bilioni 304 ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya shule za Sekondari na shule shikizi jumla 15,000 pamoja na mabweni.
Ameendelea kufafanua kuwa ujenzi wa madarasa ya shule za sekondari yatawezesha wanafunzi wote 907,803 waliofaulu mitihani ya kumaliza darasa la saba na kuingia kidato cha kwanza kuanza shule siku moja badala ya kuwa na awamu tatu kama ilivyokuwa mika iliyopita
Waziri Ummy amesema kuwa Ofisi ya Rais TAMISEMI iliomba madarasa 12,000 ikiwa na makadirio kuwa watoto watafaulu kwa asilimia 90 lakini matokeo ya mitihani ufaulu ni asilimi 82 hivyo kuna madarasa ya ziada 2,292 ambayo yatasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi wa vidato vingine katika shule za Sekondari.
Kuhusu ujenzi wa madarasa 3000 ya shule shikizi Waziri Ummy amesema serikali imewasaidia watoto wa umri mdogo kutembea umbali mrefu, kupata elimu katika madarasa mazuri na ya kisasa badala ya madarasa ya nyasi, yaliyotengenezwa na miti na ambayo hayavutii.
“Kwa upande kwa elimu msingi tumepokea fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni 50 katika shule za msingi zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum ambayo yatasadia kuboresha mazingira ya watoto wenye ulemavu kuweza kujifunza na kusoma katika mazingira mazuri” amesisitiza Waziri Ummy
Ofisi ya Rais TAMISEMI imeidhinishiwa kiasi cha shilingi bilioni 512 kupitia mpango wa maendeleo wa taifa na mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO kwa ajili ya Sekta ya Elimu, Afya na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.
No comments