Breaking News

TAKWIMU ZA UVIKO 19 KUANZA KUTOLEWA KILA WIKI KUHAMASISHA CHANJO

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea dozi Laki 8 (800,000) za chanjo ya UVIKO-19 aina ya Sinopharm kutoka Serikali ya watu wa China  ambazo zitakazo tumika kuchanja wananchi Laki 4 (400,000).

Akizungumza katika hafla ya kupokea chanjo hizo Jijini Dar es salaam, Waziri wa Afya Mhe Ummy Mwalimu amesema hadi sasa Tanzania imepokea jumla ya dozi 8,821,210 zikijumuisha aina ya Sinopharm, Janssen, Moderna na Pfizer ambazo zinatosha kuchanja jumla ya watanzania 5,082,380.

Waziri Ummy amebainisha kuwa kuwa hadi sasa jumla ya watu 1,922,019 wamechanja ambao ni sawa na asilimia 3.3 pekee ya watanzania na kuongeza kuwa  mpaka kufika tarehe 23 Januari,2022 jumla ya watu 33,000 wamethibitika kuwa na maambukizi ya UVIKO-19 na watu 781 wamepoteza maisha.
Amesema kuwa asilimia 95 ya watu waliolazwa katika hospitali mbalimbali nchini kati ya kipindi cha Septemba, 2021 hadi Januari 23, 2022 walikuwa hawajapata chanjo ya UVIKO-19 na watu waliolazwa ni 3,147 huku kati ya hao 2,990 walikuwa ni ambao hawajachanja ambapo kipindi hicho vimetokea vifo 76 na 73 kati yake walikuwa hawajachanja.

"Waliokuwa mahututi {ICU} Januari 23 pekee walikuwa 31 na kati yao 30 walikuwa hawajachanja,kwa hiyo ni vizuri watu wapime katika hili, waliopata chanjo si wengi kama waliopata" Amesema Waziri Ummy 
Aidha amemuagiza Mganga Mkuu wa Serikali kutoa takwimu za  UVIKO-19 kila wiki ili kuongeza chachu kwa wananchi kupata chanjo kwa hiyari na kuongeza kuwa chanjo zimethibitishwa ubora na usalama na kwamba tangu zimeanza kutolewa nchini hakuna kisa chochote kilichoripotiwa mtu kupata madhara. 

Amewahimiza Watanzania kuepuka matumizi holela ya dawa za 'antibiotics' kwani zinaweza kuzua janga jingine la usugu wa dawa dhidi ya vimelea vya magonjwa. Amewasihi kufika vituo vya kutolea huduma za afya kupima kwa kuwa si kila homa au mafua ni UVIKO 19

Kwa niaba ya Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassani Waziri Ummy ameishukuru Serikali ya China kwa kuwezesha upatikanaji wa chanjo ikiwa ni awamu ya pili kwa chanjo za aina ya Sinopharm awamu ya kwanza ilipokea jumla ya dozi 500,00 ambazo zilitumika kuchanja wananchi 250,000.
 

No comments