MH MAHAWANGA: ASHIRIKI KONGAMANO LA AMKA KIJANA NA UJASIRIAMALI
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es Salaam Mh. Mahawanga Janeth ameshiriki kama Mgeni Rasmi katika Kongamano kubwa la Amka Kijana na Ujasiriamali lililoandaliwa na Taasisi ya Tuamke pamoja Tanzania lililofanyika katika Ukumbi wa Check point Pugu - Mustapha.
Katika Kongamano hilo lililohudhuriwa na vikundi mbalimbali vya wajasiriamali vijana kutoka Kata mbalimbali ndani ya jimbo la Ukonga hususani wanawake na Taasisi mbalimbali ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Mh. Mahawanga amefurahishwa kuona vikundi vipya vya mabinti kwa jinsi walivyojipanga kuhakikisha wanatimiza ndoto zao katika kubadilisha uchumi wao na kutengeneza ajira kupitia ujasiriamali ambapo ameahidi kuendelea kuwa nao sambamba kuhakikisha wanapata elimu ya Fedha, Ujasiriamali, Matumizi bora ya Teknolojia ya mitandao ya kijamii ili kuweza kuwasaidia kupata fursa mbalimbali za ndani na nje ya Nchi.
Lakini pia amewahamasisha mabinti hao kuhakikisha wanawekeza kwenye kujifunza na kufanya kazi kwa bidii sambamba na kudumisha upendo, amani na mshikamano baina yao hata watakapopata mafanikio.
Aidha Mh. Mahawanga amesisitiza wazazi hasa wakinamama kuwashirikisha mabinti zao kwenye shughuli za vikundi vyao vikongwe ili waweze kujifunza zaidi masuala ya ujasiriamali na namna bora ya kuwainua kiuchumi maana kufanya hivyo kutasaidia sana kubadilisha uchumi wa mabinti kupitia shughuli za ujasiriamali na fursa zinazotuzunguka ndani ya Mkoa wetu wa Dar es Salaam.
Mh. Mahawanga amempongeza Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kufanya kuhakikisha Taifa letu linapata maendeleo na amewasisitiza vijana kumuunga mkono maana ana dhamira ya dhati ya kuleta maendeleo.
No comments