Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa Watakiwa Kusimamia Kwa Karibu Shughuli za Uchimbaji Madini
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa Nchini kuhakikisha wanatembelea maeneo yote yenye shughuli za uchimbaji wa madini na kutatua changamoto ili Sekta ya Madini izidi kukua na kuwa na mchango mkubwa zaidi kwenye uchumi wa nchi.
Mhandisi Samamba ametoa agizo hilo leo kupitia kikao cha menejimenti ya Tume ya Madini na maafisa madini wakazi wa mikoa kilichofanyika kwa njia ya video conference jijini Dodoma.
Amesema kuwa ni vyema maafisa madini wakazi wa mikoa wakahakikisha wanafahamu kila kinachoendelea katika mikoa yao hususan kwenye shughuli za madini badala ya kupata taarifa kutoka vyanzo vingine.
Katika hatua nyingine, amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kuhakikisha wanaendelea na zoezi la kuhakikisha mialo yote imesajiliwa pamoja na kuisimamia kwa karibu zaidi ili Serikali iweze kupata mapato yake.
Akielezea mikakati ya Tume ya Madini kwenye ukusanyaji wa maduhuli kupitia madini ujenzi, Mhandisi Samamba amesema kuwa Tume kupitia ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa imeshaanza zoezi la kukusanya kodi kutokana na madini ujenzi kwa kutumia mashine za kieletroniki hali itakayowezesha kukusanya fedha zaidi.
Amefafanua kuwa mafunzo ya matumizi ya mashine hizo yameshaanza kutolewa na Kitengo cha TEHAMA chini ya Kurugenzi ya Leseni na TEHAMA.
"Lengo letu kama Taasisi ni kuhakikisha tunavuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka wa fedha 2021-2022 tulilopewa la shilingi bilioni 650 ambalo tunaamini tutalivuka kabisa, kinachohitajika ni ubunifu, uzalendo na uchapakazi," amesisitiza Mhandisi Samamba
No comments