Breaking News

Katibu Mtendaji Tume Ya Madini Apongeza Ukusanyaji Wa Maduhuli Kwa Mwaka Wa Fedha 2020/21, Awataka watumishi Kuendelea Kuwa Wabunifu Na Waadilifu

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amepongeza watumishi wa Tume Makao Makuu pamoja na kwenye Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa muduhuli ambapo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021 Tume ya Madini ilipangiwa lengo la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 526.7 na kufanikiwa kukusanya shilingi bilioni 584.8

Mhandisi Samamba ametoa pongezi hizo kwenye semina ya mafunzo kuhusu namna ya kubaini na kuzuia vihatarishi vinavyokwamisha utendaji wa majukumu ya Tume ya Madini ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa maduhuli iliyoshirikisha wawakilishi kutoka Tume ya Madini Makao Makuu, Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa na Maabara ya Tume ya Madini iliyofanyika mkoani Singida.
Amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Tume ya Madini, kumekuwepo na ongezeko kubwa la ukusanyaji wa maduhuli kwa kila mwaka wa fedha ikiwa ni pamoja na ukuaji wa mchango wa sekta ya madini kwenye pato la Taifa.

"Siri ya kufanya vizuri kwenye ukusanyaji wa maduhuli imetokana na ubunifu uliooneshwa na watumishi kwenye ukusanyaji wa maduhuli na uadilifu, hivyo ninawataka kuendelea kuchapa kazi na kuhakikisha lengo tulilopangiwa la kukusanya shilingi bilioni 650 katika kipindi hiki cha mwaka wa fedha 2021/2022," amesisitiza Mhandisi Samamba.
Katika hatua nyingine, amewataka washiriki wa semina kutumia ujuzi watakaoupata katika  mafunzo hayo kuwa jicho la Tume ya Madini katika kubaini viashiria hatarishi na kuushauri uongozi wa Tume namna ya kutatua kabla ya athari kujitokeza.

Aidha, amewataka wawakilishi hao mbali na kuwa mabalozi kwenye ofisi zao kujipanga na vihatarishi vya asili kama vile ajali  na majanga kwenye migodi, na magonjwa kama vile UKIKO 19 kwa kuweka mikakati ya kukabiliana navyo.
Aidha, ameshukuru kwa ushirikiano kwenye usimamizi wa sekta ya madini ambao umekuwa ukitolewa na Waziri wa Madini, Doto Biteko, Naibu Waziri wa Madini, Profesa Shukrani Manya, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Makamishna wa Tume na menejimenti na watumishi wote.

Awali akizungumzia mafunzo hayo, Meneja wa Mipango na Utafiti wa Tume ya Madini, Andendekisye Mbije amesema kuwa lengo la mafunzo ni kuwajengea uwezo washiriki kuhusu namna ya kuainisha na  kuzuia vihatarishi vinavyoweza kukwamisha utekelezaji wa malengo ya Tume ya Madini.
Ameongeza kuwa mara baada ya kumalizika kwa mafunzo ya siku mbili, utekelezaji wake unatarajiwa kuanza mara moja katika mwaka huu wa fedha 2021-2022.

Ameongeza kuwa, utekelezaji huu ni takwa la kisheria kama linavyoelekeza na ustawi wa Tume ya Madini.
Katika hatua nyingine  Mbije amesema kuwa sambamba na mafunzo hayo, washiriki watapata fursa ya kupitishwa katika Mpango Mkakati wa Tume ya Madini wa mwaka 2019/2020 - 2023/2024 ambao unatoa dira pamoja na malengo ili kutoa uelekeo wa Taasisi katika kipindi cha utekelezaji wake.
.

No comments