Breaking News

Wekezeni Zaidi Katika Elimu ya Biashara;

SERIKALI imekutana na wajasiriamali wadogo Mkoani Dar es Salaam kutambua changamoto mbalimbali zinazowakabili wadau hao ili kustawisha vema mustakabali wa biashara zao.

Alisema elimu ya biashara ni jambo muhimu kwa wadau hao ambapo itawasaidia kukua na kuimarika kitaifa na kimataifa na kupelekea biashara hizo kufanyika kwa weredi mkubwa.

Akizungumza katika kikao maalumu na wajasiriamali hao afisa habari na mahusiano ambae alimwakilisha Mkurugenzi wa jiji la Ilala Tabu Shaibu alisema serikali ipo pamoja na wajasiriamali wadogo katika kuwahakikishia wakifanya shughuli zao katika mazingira bora.

"Serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania kupitia kwa Rais Samia Suluhu Hassan inathamini mchango wa wajasiriamali wadogo kwa kuwafanyia mambo mbalimbali ikiwemo kuwaboreshea masoko  yanapelekea kufanyika kwa mpangilio na usalama shughuli za kiashara," alisema Tabu

Aidha Tabu alieleza kwamba serikali imejipanga kuyafikia makundi mbalimbali ya wafanyabiashara wadogo kwa minajili ya kuwapa elimu ya masuala ya kibiashara ili waweze kukua na kuelewa namna ya kuendesha shughuli hizo kwa ufanisi.

Hata hivyo afisa huyo alidai kuwa kupitia rasilimali fedha wamejipanga kuhakikisha halmashauri zote za mkoa wa Dar es Salaam zinawafikia wajasiriamali wadogo kwa kuwawezesha kupata mikopo isiyo kuwa na riba na kuwataka walichukua mikopo hiyo kuirejesha kwa wakati.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya JACHI FOOD PRODUCT inayotoa huduma za chakula ameishukuru serikali kwa kuweza kukutana na kundi la wajasiriamali wadogo kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la kufikisha changamoto zao ili waweze kufanya biashara zenye tija.

Alisema kadhia ya miundo mbinu mibovu imekuwa  ikiathiri kwenye baadhi ya masoko na kupelekea kuhatarisha ustawishaji wa biashara hizo kwa vipindi tofauti hivyo waomba serikali kuliangalia hilo kwa macho mawili.

Miongoni mwa waliohudhuria kikao ni pamoja na vikundi mbalimbali vya baba na mama lishe, wawakilishi kutoka kwenye masoko ya Magomeni, Kisutu, Buguruni na Ilala mwakilishi kutoka jeshi la polisi usalama barabarani na maafisa wa biashara.
 

No comments