Breaking News

TPDC Yapongezwa Kusaidia Kuboresha Miradi ya Maji, Elimu na Afya


WANAVIJIJI wa viijiji vya Tambani wilayani Mkuranga na Nyamwimbe wilayani Kibiti Mkoa wa Pwani wamelishukuru Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) kwa kuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia kuboresha na kuwezesha upatikanaji wa huduma za maji safi na salama, elimu na huduma za afya endelevu.

Pongezi hizo wamezitoa kwa nyakati tofauti wilayani humo wakati shirika hilo likikabidhi miradi mbalimbali ambayo limekuwa likifadhili ili iweze kuwanufaisha wananchi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo maeneo inapopita miundombinu ya gesi asili.

Mwanakijiji wa Kijiji cha Tambani, Said Seif wakati akishuhudia ugawaji wa vitanda kwa ajili ya wanafunzi watakaolala bweni Shule ya Sekondari Tambani ambavyo vilitolewa na TPDC anasema, heshima wanayopata kutoka shirika hilo inazidi kuwapa hamasa ya kuendelea kuwa walinzi wakubwa wa miundombinu inayopitisha gesi asilia.

Naye Aisha Juma ambaye ni mwanakijiji wa Kijiji cha Nyamwimbe anasema, kuchimbiwa kisima cha maji safi na salama katika Zahanati ya Kijiji ni moja ya hatua kubwa ya maendeleo, kwani “TPDC imetutua sisi akina mama wa Nyamwimbe ndoo kichwani”. Sasa maji tunapata saa 24 tena mengi na ya uhakika,”anasema.

Kwa upande wa TPDC wanasema, wataendelea kusaidia jamii kwa kushirikiana na Serikali katika vipaumbele vyake vya maendeleo mchini ili kufikia malengo ya uchumi wa kati.

Meneja Mawasiliano TPDC, Marie Msellemu kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wakati wa kukabidhi misaada katika Wilaya ya Mkuranga na Kibiti mkoani Pwani anasema, shirika hilo limekuwa na utamaduni wa kurejesha kwa jamii sehemu ya mapato yao.

“Tumekuwa na utamaduni wa kutoa misaada mbalimbali hasa katika vipaumbele vya Serikali, ambavyo ni elimu,afya na maji. Huu ni utamaduni wetu wa kurudisha sehemu ya faida kwa jamii kwa ajili ya maendeleo yetu hasa katika maeneo ambayo yamepitiwa na huduma yetu ya bomba la petroli,ikiwa ni sehemu ya kusaidia Serikali kuelekea uchumi wa viwanda,”anasema Msellemu.

Meneja huyo akiwa katika Shule ya Sekondari Tambani wilayani Mkuranga walipotoa msaada wa vitanda 40 vyenye uwezo wa kulaza wanafunzi 80 vikiwa na thamani ya sh.milioni 14.4 anasema, wataendelea kushirikiana na wananchi pamoja na uongozi wa shule hiyo wakati wote kwa ajili ya maendeleo ya elimu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mkuranga, Mhandisi Mshamu Munde (wa tatu kushoto) akipokea mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni 14.4 kutoka kwa Meneja Mawasiliano TPDC, Marie Msellemu (kulia). Fedha ambazo zimetumika kununulia vitanda kwa ajili ya bweni la wasichana Shule ya Sekondari Tambani.

“Nitoe rai kwenu wanafunzi, hakikisheni mnasoma kwa bidii ili tuweze kuwapata kina mama Samia wengi ambao watalitumikia Taifa letu, pia someni kwa bidii sana masomo ya sayansi ili tuweze kupata wahandisi wengi ambao TPDC na taasisi nyingine zinawahitaji, pia tuko pamoja tukishirikiana na Serikali hasa katika upande wa elimu,ilikufikia ndoto za kuwa na taifa la watu wasomi watakaoendesha uchumi wa katika kama yalivyo malengo ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli,”anasema Meneja huyo.

Anasema, wanatambua changamoto ambazo wanafunzi wamekuwa wakizipata hasa kutembea umbali mrefu kwa watoto wa kike ndio maana hawakusita kutoa mchango huo kwa ajili ya bweni maalum la watoto wa kike.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mkuranga, Mhandisi Mshamu Munde amewapongeza TPDC kwa kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya kwa kuisaidia Serikali hasa katika wilaya hiyo huku akisisitiza kuwa wataendelea kuilinda miundombinu ya shirika muda wote.

“Serikali inawapongeza na kuwashukuru kwa misaadaa mbayo mmekuwa mkiitoa kwa muda mrefu hasa katika maeneo yaliyopitiwa na bomba lenu,na tunaahidi kuendelea kuwaunga mkono ikiwemo kulinda miundombinu yenu muda wote,”anasema Mkurugenzi huyo.

Pia Mkurugenzi huyo anawataka viongozi wa shule,wananchi pamoja na wanafunzi kutunza vitanda hivyo na mabweni kwa ajili ya maendeleo yao na kushirikiana kutatua changamoto ndogondogo zinazojitokeza.
Baadhi ya wanafunzi, walimu, watumishi wa halmashauri, TPDC wakiwa katika picha ya pamoja na mfano wa hundi waliyokabidhiwa na Meneja Mawasiliano TPDC, Marie Msellemu (kulia).

Wakati huo huo, Meneja Msellemu amekabidhi mradi wa maji katika Zahanati ya Kijiji cha Nyamwimbe kilichopo Kata ya Mlanzi Wilaya ya Kibiti Mkoa wa Pwani ambao umegharimu zaidi ya sh. milioni 21.71, fedha ambazo zilitolewa na shirika hilo.

Msellemu anasema, TPDC wanaendelea kushirikiana na Serikali hasa katika kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani.

“Tunajua muhimu wa maji katika maisha ya binadamu, hivyo tunawakabidhi mradi huu wa maji uliokamilika kwa maji ya kutosha kwa ajili ya maendeleo yenu katika shughuli mbalimbali binafsi na serikali, huu mradi katika hii zahanati ni muhimu sana, maana utakuwa umempunguzia mama kero ya maji kila wanapokuja kujifungulia hapa,” Alisema Msellemu.
Baadhi ya wawakilishi wa Kijiji cha Nyamwimbe, Halmashauri ya Kibiti na TPDC wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukabidhiwa mradi wa maji katika Zahanati ya Nyamwimbe na shirika hilo.

Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibiti, Milongo Sanga ameishukuru TPDC kwa msaada huo wa ujenzi wa mradi wa maji ambao alisema, utakuwa msaada mkubwa kwa wanakijiji hao.

“Tunawashukuru pia kwa kukubali ombi letu la ujenzi wa nyumba ya Mganga kw akuanzia kiasi kilichokuwa kimebaki cha sh.milioni 6, zilizobaki katika ujenzi wa mradi huu, tunawashukuru sana, kwani mmekuwa mstari wa mbele katika kusaidia miradi mingi ya maendeleo wilayani hapa,” Alisema.

Pia anasema, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa TPDC ili kuendelea kuwasaidia wananchi katika changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyamwimbe, Tito Manyama Msiba anasema, mradi huo wa maji katika zahanati hiyo utakuwa wa baraka zaidi kwa wanakijiji na wagonjwa wanaofika zahanati hapo.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Tambani, Mohamed Issa anasema,vitanda hivyo vimesaidia kufikia lengo kwa asilimia 95 kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi wa kike kulala bwenini shuleni hapo ili kujisomea kwa uhuru zaidi.

Na Godfrey Ismaely