Rais Magufuli: EAC Tunaweza Kujitegemea
Na Lilian
Lundo – MAELEZO,Dodoma
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Wanaafrika
Mashariki kujiamini kuwa wanaweza kutekeleza miradi ya maendeleo bila kutegemea
mataifa mengine.
Rais Dkt.
Magufuli ameyasema hayo leo Mjini Dodoma alipokuwa akihutubia Bunge la
Nne la Jumuiya ya Afrika Mashariki linalofanyika mkoani humo kwa mara
kwanza tangu kuanza kwa Bunge hilo.
“Ninazungumza
hili si kwamba hatuhitaji msaada au hatuhitaji ushirikiano, lakini ni lazima
tuliweke hili wazi, kwamba tukiamua tunaweza na mifano ipo mingi ikiwemo
Tanzania”. Alisisitiza Mhe. Rais Dkt. Magufuli.
“Tanzania
tunajenga reli ya kisasa yenye urefu wa kilometa 700.26 kutoka Dar es Salaam
hadi Dodoma kwa thamani ya shilingi Trilioni 7.6, tumeweza kununua ndege sita
na pia tumejenga meli kubwa katika Ziwa Victoria bila kuomba mkopo popote,”
amesema Rais Magufuli.
Aidha,
Rais Magufuli ameongeza kuwa wabunge wa Afrika Mashariki wanaowajibu wa
kuhakikisha wanalinda na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana ndani ya Jumuiya
hiyo.
Akitaja
baadhi ya mafanikio yaliyopatikana na Jumuiya hiyo Rais Magufuli amesema kuwa
kabla ya kuanza kwa umoja wa forodha mwaka 2005 biashara kati ya nchi wanachama
ilikuwa na thamani ya dola za kimarekani bilioni 1.8 lakini baada ya kuanzishwa
kwa umoja wa forodha imeongezeka hadi kufikia zaidi ya dola za kimarekani
bilioni 5.
Mbali na
hayo Rais, Magufuli ameshukuru uamuzi wa bunge hilo kufanyika mjini
Dodoma ambapo kwa sasa Serikali imehamishia shughuli zake zote katika mkoa huo,
na tayari watumishi wa serikali zaidi ya 3000 wameshahamia huku Rais Magufuli
akitarajiwa kuhamia muda wowote mwaka huu.
Kwa
upande wake Spika wa Bunge la Afrika Mashariki Dkt. Martin Ngoga amesema Bunge hilo
linasubiri marekebisho ya mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ili
lugha ya Kiswahili ianze kutumika kama lugha rasmi katika vikao vya bunge hilo
na katika jumuiya hiyo kwa kuzingatia azimio lililokwishapitishwa.
“Hatuoni
sababu ya kutumia lugha za wageni wakati kuna lugha yetu ambayo tunazungumza
ambayo ni kiswahili,” alisema Dkt. Ngoga.
Bunge la
Afrika Mashariki linaendelea na vikao vyake mkoani Dodoma katika ukumbi mdogo
wa Bunge wa Pius Msekwa. Bunge hilo limefanyika kwa mara ya kwanza mkoani humo.
No comments