Kutoka Muleba: Mgombea udiwani Wa CHADEMA Atoweka
WAKATI
kampeni za ubunge na udiwani zikiendelea,mgombea udiwani (Chadema) Kata ya
Buhangaza wilayani Muleba amepotea katika mazingira ya kutatanisha.
Imeelezwa
alipotea Februari 2,2018 alipokuwa akitokea Bukoba mjini kwenda nyumbani kwake
Kijiji cha Buhangaza ikidaiwa ametekwa.
Kaimu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Isack Msangi amethibitisha kupokea taarifa za
kupotea kwa mgombea huyo.
Amesema
kuwa hawana madai kuwa ametekwa bali aliondoka nyumbani na hajarejea.
Msangi
amesema polisi inawaomba wananchi kutoa ushirikiano bila kupotosha au kuegemea
upande mmoja wa kisiasa kwa kutuhumu upande mwingine bali waungane kufanikisha
kupatikana kwake.
Katibu wa
uenezi wa Chadema jimbo la Muleba Kusini na mratibu wa chama hicho jimbo la
Muleba Kaskazini, Hamisi Yusufu alisema jana Februari 4,2018 kuwa mgombea huyo
ni Athanasio Makoti (28).
Yusufu
alisema Makoti ambaye ni Mchungaji wa Kanisa la AGT anashiriki uchaguzi mdogo
wa udiwani utakaofanyika Februari 17. Anachuana na mgombea wa CCM, Jenitha
Tibeyenda na wa NCCR -Mageuzi, Grason Anaseti.
Alisema
Februari 2,2018 saa 12:00 jioni akitumia simu yake ya mkononi aliwajulisha
viongozi wa Chadema ngazi ya wilaya kuwa alipanda gari lenye watu wanne kutoka
Kijiji cha Mafumbo njia panda ya kwenda Kamachumu akielekea Kijiji cha
Buhangaza.
Yusufu
alisema baadaye ujumbe mfupi wa maneno (sms) ulitumwa kwa Advera Kalikwela,
diwani wa viti maalumu (Chadema) Kata ya Ijumbi ukieleza, “Nimeteremka hapa
Mafumbo kabla ya kufuatwa na bodaboda wangu nimezingirwa na gari lenye watu
wanne mmoja mwanamke, mbele dereva wa kiume na vijana wengine wawili ni kama
nimetekwa.”
Alisema
baada ya ujumbe huo, simu ya Makoti iliita bila kupokewa na hadi sasa hakuna
taarifa za kuonekana kwake na kwamba familia ilitoa taarifa polisi.
Egbert
Makoti ambaye ni mdogo wa mgombea huyo amesema baada ya kuchukua fomu, ndugu
yake aliwaeleza kuna watu ambao hakuwataja waliomtaka aachane na kata hiyo
wakimtaka apokee Sh8 milioni lakini alikataa.
Katibu wa
Baraza la Wazee la Chadema, Rodrick Lutembeka amesema chama hicho kitaendelea
kumnadi katika kampeni zinazoendelea katika Kata ya Buhangaza.
Kata hiyo
ina vijiji vitatu vya Buhangaza, Kashenge na Buyaga ikiwa na vitongoji 13
ikikadiriwa kuwa na zaidi ya wapiga kura waliojiandikisha 2,500.
No comments