Haya Ndio Maamuzi ya Mahakama Ya KISUTU Kwa Raia Wa Uganda Aliekuwa Akisafirisha Dola Milioni 1 Uwanja Wa Ndege JNIA.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu
raia wa Uganda, Winfred Businge kulipa faini ya Sh100 milioni au kutumikia
kifungo cha miaka mitatu jela.
Businge (33), amelipa faini hivyo kukwepa
kifungo. Hukumu imetolewa leo Jumanne Februari 6,2018
na hakimu mkazi mkuu, Huruma Shaidi baada ya mshtakiwa kukiri kosa.
Mshtakiwa alifikishwa mahakamani akidaiwa
kuingiza nchini dola 1 milioni za Marekani (Sh2.2 bilioni) bila kutoa taarifa
kwa mamlaka ya forodha.
Businge anadaiwa kutenda kosa hilo Desemba
11,2017 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar
es Salaam.
Kesi hiyo ilikuwa ikiendeshwa na wakili wa
Serikali mwandamizi, Awamu Mbagwa na mshtakiwa aliwakilishwa na wakili Hudson
Ndusyepo.
Mshtakiwa aliposomewa shtaka kwa mara ya
kwanza alikana na alikuwa nje kwa dhamana.
Kwa mara ya kwanza, Rais John Magufuli Desemba
13,2017 alizungumza kuhusu fedha hizo alipokuwa akifungua tawi la Benki ya CRDB
mjini Dodoma.
No comments