Chadema Hatuna Imani Na Msimamizi Wa Uchaguzi Kinondoni
Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kimemkataa msimamizi wa uchaguzi wa ubunge jimbo la Kinondoni kwa
madai kuwa ameshindwa kusimamia taratibu za uchaguzi.
Pia, chama hicho kikuu cha upinzani
nchini kimemwandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro na
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wakikituhumu CCM kuandaa mikakati ya
kufanya vurugu siku ya uchaguzi huo, Februari 17.
Hayo yameelezwa leo Februari 6, 2018
na Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Chadema, Benson Kigaila katika
mkutano wake na waandishi wa habari.
Kigaila amesema mwenendo wa uchaguzi,
hasa kamati ya maadili ya Kinondoni inayoongozwa na Mkurugenzi wa Manispaa
hiyo, Aron Kagurumjuli inasimamia mambo isiyoyahusu.
Amesema malalamiko yanayotolewa ni ya
kijinai na hayawezi kufanyiwa kazi na kamati ya maadili, “Kimsingi kamati ya
maadili haina uwezo nayo, yanapaswa kupelekwa polisi yenye jukumu ya kufanya
uchunguzi.”
"Kamati ya maadili
haishughulikii masuala ya jinai, watu wakipiga, wakipigwa wanashughulikiwa na
polisi. Mkurugenzi ni msimamizi wa uchaguzi lakini amekuwa akiyashughulikia
kinyume cha kanuni," amesema.
Alisema katika barua hiyo wameeleza
mienendo ya mkurugenzi huyo wakidai kuwa si mizuri, “Hatumkubali, hatumtaki,
aondolewe na tunapinga kwani hawezi kutenda haki.”
Alisema suala la jinai ambalo
Kagurumjuli analishughulikia ni la madai ya mwanachama wa CCM kupigwa na
vijana wa Chadema, “Hatujajua hao vijana wanaotuhumiwa ni wa Chadema au la
lakini hata kama ni kweli, mwanachama mmoja huwezi kuiwajibisha Chadema."
Katika mkutano huo, Kigaila amedai
CCM wameanza kuandaa vijana kufanya vurugu katika uchaguzi huo na
kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua.
"Tumeandika barua kwa IGP na
NEC. Tumesema yeyote atakayejeruhiwa CCM iwajibike kwani imeanza kusambaza
silaha, mashoka, nondo na mapanga," amedai Kigaila na kwamba barua hizo
wanazipeleka leo katika taasisi hizo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Operesheni ya
Kampeni Kinondoni, Frederick Sumaye amesema tuhuma hizo ana imani zitafanyiwa
kazi.
Waziri Mkuu huyo wa zamani amesema
jitihada kubwa zinapaswa kufanyika nchini ili nchi kutoondolewa katika mfumo wa
vyama vingi kwa madai kuwa vyombo vinavyosimamia uchaguzi vinahakikisha
wapinzani hawashindi.
"Tunaitaka NEC katika chaguzi
hizi itende haki, Polisi wanaosimamia amani wote watende haki ili uchaguzi
ufanyike kwa amani. Wasimamizi wa uchaguzi watende haki," amesema Sumaye.
No comments