Waziri Mkuu Majaliwa Atoa Onya Kwa Mawaziri kutumia Vizuri Madaraka Yao
Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa amewaonya mawaziri na kuwataka watumie madaraka yao kwa manufaa ya
Taifa na kamwe wasiyatumie kama fursa ya kujitajirisha wao binafsi.
Kassim Majaliwa amesema
hayo leo Oktoba 16, 2017 alipozungumza na baadhi ya Mawaziri, Manaibu na
Makatibu Wakuu katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Aidha Waziri Mkuu amesema
Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli amesisitiza kwamba amewateua ili wafanye
kazi na kamwe wasitumie madaraka waliyopewa kwa maslahi yao binafsi.
“Madaraka haya ya Uwaziri
si fursa ya kujipatia utajiri, tunatakiwa tufanye kazi kwa weledi, uadilifu,
bidii na uaminifu mkubwa ili kuondoa kero za wananchi kwa wakati.”
Waziri Mkuu amesema
Mawaziri hao wanatakiwa wasimamie utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa Taifa
wa miaka kuanzia mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021. Pia utekelezaji wa ahadi zote
zilizopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 pamoja na ahadi alizozitoa
Rais Dkt Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi.
Hata hivyo Waziri Mkuu
amewataka Mawaziri hao wakapunguze urasimu katika utekelezaji wa malengo ya
Serikali kwa sababu wananchi wanahitaji kuhudumiwa kwa wakati
Mawaziri waliohudhuria
kikao hicho ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –TAMISEMI Bw. Suileiman Jaffo
pamoja na Manaibu wake Bw. Joseph Kandege na Bw. George Kakunda, Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi Ummy Mwalimu na Naibu wake
Dkt. Faustine Ndungulile.
Wengine ni Waziri wa Maji
na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe na Naibu wake Bw. Jumaa Aweso, Waziri wa
Viwanda na Biashara Bw. Charles Mwijabe na Naibu wake Mhandisi Stella Manyanya.
Waziri wa Maliasili na
Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla na Naibu wake Bw. Josephat Hasunga, Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako na Naibu wake Bw. William
Ole Nasha, Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Bw. Abdallah Ulega pamoja na
Makatibu Wakuu wa Wizara hizo.
No comments